info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

WANAWAKE WA TTCL WATOA MSAADA OCEAN ROAD

Tarehe 8 Machi kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake, ama Siku ya Wanawake Duniani. Katika siku hii, wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania huungana na Wanawake wenzao duniani kote kuadhimisha siku hii muhimu.

Ni katika siku hii wanawake hukutana na kujadiliana kuhusu mafanikio waliyopata katika sekta mbalimbali, changamoto wanazopitia, na jinsi ya kukabiliana na changamoto hizo.

Kwa mwaka huu Kauli mbiu ya Siku hii mwaka huu ni “Ubunifu na Madiliko ya Teknolojia:Chachu katika kuleta Usawa wa Kijinsia.” Kwa kaulimbiu hii, Dunia inataka kuona umuhimu wa Mwanamke kujikita katika masuala ya teknolojia na ubunifu, ili kuweza kuendelea kutimiza ndoto zao katika nyanja mbalimbali.

Ni wakati sasa kwa wanawake na wasichana kuitumia vyema teknolojia kujikwamua katika masuala ya kujiimarisha kiuchumi kupitia ubuni wa kazi na shughuli mbalimbali za ujenzi wa Taifa na familia kwa ujumla.

Kihistoria siku hii huadhimishwa lengo likiwa ni kumkumbusha matokeo ya kisiasa, kijamii, kiuchumi waliyofikia wanawake, msimamo wa imara katika ngazi ya jamii na kuongeza chachu katika harakati za mapambano katika usawa wa kijinsia.

Kipekee Wanawake wa Shirika la Mawasiliano Tanzania hutumia maadhimisho haya kufanya shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na kufanya usafi katika maeneo ya hospitali, kuchangia damu, kutoa zawadi kwa makundi yenye mahitaji maalum kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya kibinadamu.

Kwa mwaka huu wa 2023 wanawake wa TTCL wameshiriki katika maadhimisho hayo yaliyofanyika ngazi ya Mkoa, hadi Taifa na kuhusisha wanawake wa Taasisi, kampuni, mashirika na makundi maalum ya kina mama kwakubeba mabango yenye ujumba mbalimbali kuendana na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu.

Aidha wanawake hao wameyatumia maadhimisho hayo kuwatembelea wagonjwa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road jijini Dar es Salaam. Wakiwa hospitalini hapo wanawake hao wamekabidhi vifaa mbalimbali ikiwa ni pamoja na Pampasi Katoni 30, Sabuni ya unga viroba 7, mafuata ya kupaka katoni 4, Sabuni ya mche katoni 7 na pamoja na Dawa ya meno katoni 10 ikiwa ni sehemu ya namna ya kipekee kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani huku lengo likiwani kuwapa pole wagonjwa na kuwapongeza wafanyakazi na watoa huduma kwa kazi wanayoifanya katika kuwahudumia wagonjwa hospitalini hapo.

Pamoja na matendo hayo ya huruma wamepata fursa ya kuwatembelea wagonjwa katika wodi tofauti tofauti na kuzungumza nao kwakuwapa neno la faraja.

Katika hatua nyingine Wanawake hao wametoa shukrani za dhati kwa Menejimenti ya TTCL kwakuendelea kuunga mkono maadhimisho haya ambapo shirikia hutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha malengo yaliyokusudiwa na kundi hilo la wananwake ndani ya shirika.

Kihistoria Siku ya Wanawake Duniani kwa mara wa kwanza ilisherehekewa mwaka wa 1911 ambapo mataifa kumi na moja yalikusanya wanawake mia moja walipoanza kuadhimisha siku hii. Mwaka 1908 jumla ya wanawake elfu kumi na tano waliandamana katika katika mji wa New York wakidai kupunguziwa muda wa kufanya kazi, kupata ujira wa kuridhisha na kupewa haki ya kupiga kura. Mwaka 1909 mwanamke kwa jina la Clara Zetkin alipendekeza kuanzishwa kwa Siku ya Wanawake Duniani katika Mkutano wa Wafanyakazi Wanawake uliofanyika katika jiji la Copenhagen nchini Denmark.