info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

HAKUNA UCHUMI WA KIDIGITALI BILA TTCL KUWAJIBIKA- KM ABDULLAH

SERIKALI ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, imelitaka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TCCL), kuhakikisha linaendelea kuleta mageuzi katika sekta ya teknologia nchini ili kufikia uchumi wa kidijitali.

Katibu Mkuu Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknologia ya Habari Jamuhuri ya Muungano wa Tanznzania, Mohammed Khamis Abdullah alieleza hayo wakati akifungua Kikao Kazi cha Bodi ya Wakurugenzi na Menejment ya TTCL katika hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.

Alisema shirika hilo linategemewa sana na serikali katika kufikia uchumi wa kidijitali hivyo ikiwa litawajibika ipasavyo basi litasaidia sana kufikia dhamira hiyo ya serikali.

Aidha alisema shirika hilo limepewa dhamana kubwa ya kusimamia miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano ambayo ni mkongo wa taifa wa mawasiliano na kituo cha kuhifadhi data kimtandao (NIDC) hivyo ni vyema kupanga namna bora ya kuhakikisha miundombinu hiyo inatunzwa kwa malengo ya kuleta tija iliyokusudiwa.

Alibainisha kwamba hakuna uchumi wa kidijitali Tanzania bila ya shirika hilo kuwajibika ipasavyo kwani shirika hilo limeaminiwa na serikali kuweza kuwafikishia wananchi na majirani zao kuwafikishia huduma za mawasiliano ili kufikia uchumi wa kidijitali.

“Katika kufikia Tanzania ya kidijitali moja ya nguzo muhimu ni miundombinu ya mawasiliano ambayo inasimamiwa na TTCL bila ya Shirika hili kusimamia vizuri basi ni ndoto kufikia uchumi wa kidijitali Tanzania,” alisema.

Alibainisha kuwa ni lazima uongozi wa TTCL kuhakikisha wanatoa huduma nzuri kwa wananchi hasa huduma kwa wateja kama wanavyofanya mitandao mengine ya Mawasiliano.

Hata hivyo alisema kikao hicho ni muhimu katika kuona wanatekeleza mikakati ya Shirika kwa kuzingatia maslahi ya taifa na wananchi wake kwa ujumla na kuwataka wajumbe kutumia kikao hicho kujadili changamoto zinazowakabili shirika na kuzitafutia majibu changamoto hizo   

Sambamba na hayo, aliitaka bodi hiyo kuhakikisha wanayafanyia kazi mambo mbalimbali ikiwemo la kuhakikisha ujenzi wa kilomita 1600 za Mkongo wa Taifa zinakamilika ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vipya 15 vya kutolea huduma za Mkongo wa Taifa hadi ngazi za wilaya.

Alisema Shirika hilo linapaswa kuhakikisha linatumia fursa ya uwepo wa mkongo kwa kufungua biashara nchi jirani, kuunganisha huduma za faiba mlangoni kwa kuwafikia watumiaji angalau 200,000 na kuwezesha maeneo 50 muhimu ya umma katika Miji Mikuu kupata huduma za Wi- Fi.

Katibu huyo aliisisitiza bodi hiyo kuhakikisha wanafanya tafiti na kuishauri Wizara namna bora ya kushusha gharama za huduma za mkongo ili kuvutia wateja wengi zaidi na kufanya utafiti ambao utaweza kuibua huduma zinazoambatana na matumizi ya faiba ili kuvutia watumiaji.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Zuhura Snare Muro, alisema kikao hicho kinatokana na utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kuona mashirika yakijiendesha huku yakitoa huduma bora kwa umma, na kutoa gawio kwa serikali. 

Alisema katika kuyafikia malengo hayo shirika lina mpango wa miaka mitano ili kuona inawaunganishia mawasiliano zaidi ya nyumba 100 na kuwa na Wi Fi za umma na pia katika mji wa kitalii ikiwemo Mji Mkongwe kuona wanasambaza huduma za mawasiliano ili watalii wanapokuwa waweze kupata mtandao kwa haraka zaidi. 

Mwenyekiti Zuhura alisema wanategemea kujenga minara zaidi ya 1000 na kuongeza upatikanaji wa huduma za mkongo kwa wilaya zaidi ya 71 na Zanzibar kunakuwa na mkongo huo. 

Alimpongeza Rais wa jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuzipa kipaumbele sekta ya mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata uchumi wa kidijitali.

Mbali na hayo, alisema hivi sasa Tanzania inawekeza katika gesi na mafuta, kilimo na uvuvi kwani mali nyingi zinaibiwa baharini hivyo ni lazima kuhakikisha kwamba shirika hilo linachunga maliasili za nchi na hilo litawezekana kwakutumia ‘satellite’ ambako ndiyo dira ya TTCL kuhakikisha linafika huko kiteknolojia.