BALOZI WA ANGOLA NCHINI TANZANIA ATEMBELEA BANDA LA TTCL SABASABA 2026
Balozi wa Jamhuri ya Angola nchini Tanzania, Mheshimiwa Domingos Coelho, ametembelea Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere.
Katika ziara hiyo, Balozi Coelho alipata maelezo kuhusu huduma na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazotolewa na TTCL, ikiwemo huduma za Kitengo cha Wateja Wakubwa (Enterprise Business), Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National Internet Data Centre – NIDC), huduma ya TTCL Public Wi-Fi pamoja na Call Center Business.
Aidha, alijionea namna TTCL inavyoendelea kutumia teknolojia za kisasa kuimarisha huduma za mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa intaneti ya kasi na kuwezesha utoaji wa suluhisho za kidijitali kwa taasisi za umma, sekta binafsi na wananchi.
Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mheshimiwa Domingos Coelho alieleza kufurahishwa na maendeleo makubwa ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), akibainisha kuwa ni miundombinu ya kimkakati inayowezesha upatikanaji wa huduma za mawasiliano za uhakika, salama na nafuu, huku ikichochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Alipongeza juhudi za TTCL katika kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya kisasa ya mawasiliano na teknolojia za kidijitali, akieleza kuwa maendeleo hayo yanaimarisha mazingira ya biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kikanda katika sekta ya mawasiliano.
TTCL inaendelea kutumia Maonesho ya Sabasaba 2026 kama jukwaa la kuonesha ubunifu, teknolojia na suluhisho za kisasa zinazolenga kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali na kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi na wadau mbalimbali.