BENKI YA EXIM YA CHINA YAIPONGEZA TTCL KWA UENDESHAJI BORA WA KITUO CHA TAIFA CHA UTUNZAJI DATA (NIDC)
Na Spencer Kulwa
Benki ya EXIM ya China imelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa uendeshaji bora wa Kituo cha Taifa cha Utunzaji Data kimtandao (National Internet Data Centre – NIDC), kinachosimamiwa na TTCL, hususan katika kuendana na mabadiliko ya teknolojia na kuimarisha utoaji wa huduma za kidijitali nchini.
Pongezi hizo zimetolewa leo wakati wa ziara ya ujumbe wa Benki ya EXIM ya China katika kituo hicho, ukiongozwa na Makamu wa Rais wa benki hiyo, Bw. Wang Kang, kwa lengo la kujionea shughuli za uendeshaji wa kituo na namna kinavyotekeleza majukumu yake katika kuhudumia mahitaji ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mkurugenzi wa Ufundi, Mhandisi Cecil Francis, aliwasilisha maelezo kuhusu uendeshaji wa kituo hicho, huduma zinazotolewa na namna kinavyoendelea kutekeleza majukumu yake ili kuhakikisha malengo ya kuanzishwa kwake yanafikiwa.
Kupitia ziara hiyo, ujumbe wa Benki ya EXIM ya China ulipata fursa ya kufahamu zaidi mchango wa NIDC katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini na kuwezesha utoaji wa huduma za TEHAMA zinazokidhi mahitaji ya taasisi na wadau mbalimbali.
Pongezi hizo ni ishara ya kutambua juhudi za TTCL katika kusimamia na kuendeleza miundombinu muhimu ya mawasiliano na teknolojia ya habari, sambamba na dhamira ya Shirika ya kuendelea kuboresha huduma zake kulingana na maendeleo ya teknolojia.