info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

BODI YA WAKURUGENZI TTCL YATEMBELEA NICTBB KIBAHA NA SEACOM

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imefanya ziara maalum katika kituo cha SEACOM kilichopo Dar es Salaam na Kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) cha Kibaha Mkoa wa Pwani, ikiwa na lengo la kujionea na kupata uelewa wa kina kuhusu miundombinu muhimu ya mawasiliano nchini.

Katika ziara hiyo iliyofanyika Agosti 11, mwaka huu, Bodi hiyo ilipata fursa ya kupokea maelezo ya kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa TTCL kuhusu jinsi miundombinu ya SEACOM inavyofanya kazi, umuhimu wake katika kukuza uchumi wa kidijitali, na nafasi yake katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano kwa Watanzania na nje ya mipaka ya Tanzania.

Kupitia ziara hii, Wajume walijifunza zaidi kuhusu namna mkongo unavyounganisha Tanzania na Dunia kupitia huduma ya intaneti, na namna miundombinu hiyo inavyoweza kutumika kikamilifu kuchochea matumizi ya TEHAMA katika sekta mbalimbali.

Aidha Wajumbe walipata maelezo ya kitaalamu kuhusu kituo cha SEACOM cha Dar es Salaam, namna mfumo wa nyaya za mawasiliano za chini ya bahari unavyofanya kazi na mchango wake katika kusafirisha taarifa kwa kasi na usalama mkubwa na kujifunza hatua zinazochukuliwa kuhakikisha uthabiti wa miundombinu hii ambayo ni mhimili wa mawasiliano ya kidijitali nchini.

Wakiwa katika kituo cha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kilichopo Kibaha, Wajumbe walipata maelezo ya kina kuhusu namna kituo hicho kilivyo muhimili mkubwa wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa viwango vya juu, fursa zilizopo katika kuendeleza miundombinu hiyo na jinsi shirika linavyokabiliana na changamoto katika uendeshaji wa miundombinu hiyo.

Vilevile, wajumbe walikagua mnara wa mawasiliano wa TTCL uliopo Kibaha Mkoa wa Pwani, ambao unatoa huduma za simu na intaneti katika maeneo mbalimbali, yakiwemo Chuo cha Uongozi cha Mwalimu Nyerere.

Ziara hiyo pamoja na mambo mengine ni sehemu ya jitihada za Bodi ya Wakurugenzi za kufuatilia utekelezaji wa miradi ya TTCL ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinakuwa za kisasa, zenye kasi, ubora na usalama unaokidhi mahitaji ya wananchi na kukuza uchumi wa kidijitali.