info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

HAKUNA MAPINDUZI YA TEKNOLOJIA TANZANIA BILA TTCL-MURO

Shirika la Mawasiliano Tanzania- TTCL Corporation limefanikiwa kukusanya shilingi 135,216,317,693 hadi kufikia Aprili 2024 katika Mwaka wa Fedha 2023/24 sawa na asilimia 56.34 ya lengo lililopangwa la kukusanya Shilingi 240,000,000,000 kutokana na huduma za mawasiliano, ukodishaji wa vifaa vya mawasiliano, upangishaji majengo na ruzuku kutoka Serikali Kuu. 

Hayo yalisemwa hivi karibuni na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye (Mb) wakati akiwasilisha Bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

Alisema hadi kufikia Aprili 2024 TTCL ilifanikiwa kujenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Wilaya 22 za Karatu, Mbulu, Longido, Hai, Mwanga, Pangani, Muheza, Lushoto, Kibiti, Mtama, Nachingwea, Newala, Mbinga, Ludewa, Ileje, Vwawa, Mbogwe, Msalala,Tarime, Sengerema, Rorya na Ngara.

Aidha alisema TTCL imefanikiwa kuunganisha watumiaji 12,584 wa huduma za Faiba Mlangoni sawa na asilimia 63 ya lengo.

Aliongeza kuwa Shirika limefanikiwa kuwezesha upatikanaji wa huduma ya Wi-Fi katika maeneo manne ya umma ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo cha Kilimo cha Sokoine (SUA) na Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam,"alisema Nape.

Aidha Waziri Nape alisema kuwa TTCL ilifanikiwa kufanya tafiti mbili za kuridhika kwa wateja ambapo lilisajili wateja 102,850 wapya wa T-PESA kwa ajili ya kutumia huduma za kifedha za T-PESA na kuunganisha Taasisi sita za Serikali na Binafsi kwa ajili ya huduma za malipo ya mkupuo (bulk disbursement).

Vilevile alieleza kuwa shirika hilo lilifanikisha kusainiwa kwa Mikataba ya mauzo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na nchi za Uganda wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 28.8, Malawi wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 5.5 na Kampuni ya Airtel wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 4.8.

Wakati wa uwasilishaji wa Bajeti hiyo TTCL ilikuwa na miongoni mwa Mashirika, Taasisi na Kampuni zilizochini ya Wizara hiyo zilizoshiriki maonesho ya Siku mbili Mei 16 hadi Mei 17, 2024 kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma ambapo maonesho hayo yaliandaliwa kwa ajili ya Wahe. Wabunge kupata taarifa mbalimbali za utekelezaji wa majukumu ya Wizara kupitia Taasisi hizo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), leo Mei 16, 2024 ametembelea Banda la Maonesho la Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL wakati Shirika hilo liliposhiriki maonesho ya Taasisi, Kampuni na Mashirika yaliyo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari katika Viwanja vya Bunge jijini Dodoma. 

Katika maonesho hayo TTCL kupitia Mkurugenzi Mkuu Mhandisi Peter Ulanga alipata fursa ya kumwelezea Mhe. Waziri Mkuu miradi ya kimkakati inayoendeshwa na Shirika hilo ikiwa ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo mahiri cha kutunza kumbukumbu (NIDC)

Kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano TTCL imeziunganisha nchi 8 za ukanda wa Afrika Mashariki huku zaidi ya Wilaya 92 zikiwa zimeunganishwa na Mkongo huo na hivyo kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi, Afya na kijamii kufanyika kidigitali.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo Bi. Zuhura Muro, akizungumza na vyombo vya habari jijini humo alisema kuwa hakuna mapinduzi ya kiteknolojia Tanzania bila TTCL hivyo bajeti ya Wizara hiyo itawezesha kujenge ustahimilivu wa mawasiliano kwani watahakikisha huduma za mawasiliano za uhakika zinawafikia wananchi.

" Kwanza bajeti hii ina maana kubwa sana kwetu kama shirika kwa sababu Bunge linaelewa adhma ya Rais Samia ya kutaka kuhakikisha changamoto zote za mawasiliano zinatatuliwa katika nchi yetu na kazi hiyo inafanywa na sisi TTCL," alisema Bi. Zuhura

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga alisema kuwa watanzania baada ya kuona Bajeti yao imepita kwa kishindo waamini kuwa TTCL inakwenda kuboresha miundombinu ya mawasiliano ili kufikia katika uchumi wa Kidigiti.

"Sisi tunausika na ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano hivyo watanzania ambao wameshughudia bajeti hii inapita kwa kishindo naomba wajue kwamba sisi tutajenga miundo mbinu ambayo itawawezesha wao kufikia malengo katika ukuzaji wa uchumi wa Kidigitali," alieleza Mhandisi Ulanga

.