
HONGERA WAFANYAKAZI, BIDII YA KAZI YENU IMEONEKANA- RAIS DKT. SAMIA
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka 2025 yamefanyika kwa mafanikio makubwa Kitaifa mkoani Singida, yakihudhuriwa na maelfu ya wafanyakazi kutoka katika Taasisi, Kampuni na Mashirika mbalimbali ya Umma, wakiwemo Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL waliovutia hisia za wengi kwa ushiriki wao wa kipekee.
Mgeni rasmi alikuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alitumia jukwaa hilo kutoa hotuba iliyogusa mioyo ya Wafanyakazi hasa kwa kuahidi maboresho katika maslahi ya wafanyakazi hao nchini.
Katika hotuba yake, Mhe. Dkt. Rais Samia alitoa pongezi kwa Wafanyakazi na Vyama vya Wafanyakazi kwa kufanya kazi kwa bidii hali iliyopelekea uchumi kukua kwa asilimia 5 kwa mwaka huu na hivyo kuwaahidi wafanyakazi hao kuwa serikali itaboresha maslahi yao ikiwemo kima cha chini cha mshahara.
“Sasa kwakuwa mcheza kwao hutunzwa, mimi na wenzangu na baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda kwa sababu ya nguvu zenu wafanyakazi, ninayofuraha kuwatangazia kwamba mwaka huu serikali itaongeza kima cha mshahara kwa Watumishi wa Umma kwa Aslimia 35 nukta moja” Alisema Rais Samia huku Wafanyakazi wakishangilia kwa furaha
Aidha alivipongeza vyama vya Wafanyakazi kwa ushirikiano wanaoutoa kwa serikali katika kuwasilisha changamoto za wafanyakazi na kuhakikisha zinafanyiwa kazi kwa haraka na alivihimiza vyama hivyo kuendelea kuweka juhudi za kutetea maslahi ya wafanyakazi ili waendelee kuaminiwa na kutosababisha wafanyakazi kujitoa katika vyama.
Rais Dkt. Samia aliwahakikishia wafanyakazi kuwa mapungufu yaliyobainishwa na vyama vya wafanyakazi yamepokelewa, na alitumia jukwaa hilo kuziagiza Wizara zinazohusika kufanyia kazi mapungufu hayo yakiwemo ya ajira za mikataba mifupi huku akiwahakikishia wafanyakazi kuwa serikali inaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha mazingira bora ya kazi, malipo stahiki na ulinzi wa haki zao unaimarishwa.
Katika tukio hilo, wafanyakazi wa TTCL walikuwa ni miongoni mwa Mashirika ya Umma waliyojipanga vyema, walishiriki maandamano wakiwa wamevaa sare za rangi ya ‘bluu’ zenye nembo ya shirika, huku wakibeba mabango yenye ujumbe wa kuhamasisha wananchi kutumia huduma zinazotolewa na shirika hilo pamoja na kaulimbiu kitaifa: “Uchaguzi Mkuu 2025 utuletee Viongozi wanaojali Haki na maslahi ya Wafanyakazi sote tushiriki’’,
Sherehe za Mei Mosi zilihusisha gwaride rasmi la vyama vya wafanyakazi, Vikundi vya ngoma za asili, burudani kutoka kwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya, pamoja na maonyesho ya vitendea kazi za taasisi mbalimbali na huduma na bidhaa zinazotolewa kwa wananchi.
Maadhimisho ya Mei Mosi 2025 yameacha alama kubwa si tu kwa sababu ya hotuba ya Mhe. Rais iliyojaa matumaini, bali pia kwa mshikamano uliooneshwa na wafanyakazi kutoka mashirika ya umma na binafsi ikiwemo TTCL ambao wameonesha kuwa wako tayari kuendelea kuchapa kazi kwa bidii na weledi katika kuwatumikia wananchi.
Maadhimisho ya Mei Mosi Kitaifa yalihuduhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Wafanyakazi pamoja na wafanyakazi sekta binafsi na serikali wakati huo huo maadhimisho hayo pia yalifanyika ngazi ya mikoa.