info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

KAMATI YA BUNGE YA TEHAMA NA MIONGOZO YA KITAIFA YA UGANDA YAFANYA ZIARA TTCL

Wajumbe wa Kamati ya Bunge ya TEHAMA na Miongozo ya Kitaifa ya Uganda kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano ya Uganda (NITA-U) wafanya ziara ya kujifunza kuhusu Miundombinu ya Mawasiliano.

Ziara hiyo ya siku tatu yenye lengo la kujifunza kuhusu miundombinu ya Kimkakati ya mawasiliano ilifanyika tarehe 25 Machi 2024 katika ofisi za Shirika la Mawasiliano Tanzania-TTCL Makao Makuu DSM.

Akizungumza wakati ziara hiyo Kiongozi wa Ujumbe huo Mhe. Ayoo Tony alisema wanashukuru sana TTCL kwa kukubali kuwapokea na kutoa fursa kwao kujifunza masuala mbalimbali ya TEHAMA kwani wanaamini kuwa TTCL na Tanzania kwa ujumla imepiga hatua kubwa sana katika maendeleo ya Kidijitali.
 
"Sisi ni ndugu na ushirikiano wetu ni wa muda mrefu na ni ukweli usiopingika kuwa Tanzania ipo mbali katika TEHAMA  ndiyo maana tumeona ni vyema kuja kujifunza na kupata uelewa zaidi wa uendeshaji na usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano na jinsi ya kuboresha masuala ya Kidijitali Uganda.Alisema Bw. Ayoo

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Peter Ulanga alisema TTCL ni kitovu cha maendeleo ya uchumi wa Kidijiti hapa Tanzania hivyo ni jukumu la TTCL kuhakikisha panakuwa na  miundombinu thabiti inayoweza kuhudumia maeneo mbalimbali pamoja na nchi jirani kwa ufanisi wa hali ya juu.

"Jukumu letu kama TTCL ni kuhakikisha mawasiliano bora na thabiti kwa wateja wetu na kwa sasa tunaendelea na maboresho pamoja na upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano  katika maeneo mbalimbali hivyo ni imani yetu kuwa tutaweza kutoa huduma kwa kiwango cha juu. Alisema Mhandisi Ulanga

Hadi sasa  Shirika hilo limeshaunganisha nchi mbalimbali na Mkongo wa Taifa wa mawasiliano ikiwemo Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Malawi, Zambia.