KAMISHNA MKUU WA TRA AIPONGEZA TTCL KWA USIMAMIZI BORA WA NIDC
Na Godfrey Andafiche
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Juma Mwenda, amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa weledi na ufanisi katika usimamizi wa Kituo cha Taifa cha Kutunza Data Kimtandao (NIDC), ambacho kina mchango mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali nchini.
Pongezi hizo amezitoa wakati wa ziara yake katika kituo hicho, ambapo alipata fursa ya kujionea miundombinu ya kisasa ya kiteknolojia, huduma zinazotolewa pamoja na mchango wa kituo hicho katika kuwezesha taasisi za umma na binafsi kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
“Ninaipongeza TTCL kwa usimamizi wa Kituo cha Taifa cha Kutunza Data (NIDC), ambacho kina mchango mkubwa katika kuimarisha miundombinu ya TEHAMA nchini,” amesema Kamishna Mkuu Mwenda.
Katika ziara hiyo, Kamishna Mkuu alipokelewa na Mkuu wa Kituo cha NIDC, Mhandisi Sosthenes Malimi, ambaye alimweleza kwa kina kuhusu uwezo wa kituo hicho katika kutoa huduma za uhifadhi na usimamizi wa taarifa na mifumo ya kidijitali kwa kuzingatia usalama, uhakika na uendelevu wa huduma.
“NIDC tumejidhatiti katika kutoa huduma bora, salama na za uhakika za uhifadhi na usimamizi wa taarifa na mifumo ya kidijitali,” amesema Mhandisi Malimi.
Kupitia NIDC, TTCL inaendelea kutekeleza jukumu lake la kimkakati la kuimarisha miundombinu ya kidijitali, kuwezesha taasisi kutumia teknolojia kwa ufanisi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.