info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

KIJA WAJIONEA NGUVU YA TEKNOLOJIA KATIKA KITUO CHA KIDIGITALI KIJITONYAMA

Wanachama wa Kinondoni Jogging Association (KIJA) wametembelea Kituo cha Kidigitali Kijitonyama na kujionea kwa karibu namna teknolojia za kisasa na intaneti yenye kasi zinavyoweza kubadili maisha ya wananchi, kuimarisha biashara na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma mbalimbali.

Katika ziara hiyo, wanachama hao walipata fursa ya kufahamu zaidi kuhusu huduma ya Faiba Mlangoni Kwako inayotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), pamoja na namna huduma hiyo inavyowawezesha wananchi kupata intaneti ya uhakika na yenye kasi majumbani na katika maeneo ya biashara.

Washiriki walishuhudia matumizi ya intaneti ya kasi katika kuwezesha shughuli mbalimbali za kidijitali, zikiwemo mawasiliano ya video, elimu kwa njia ya mtandao, biashara za kidijitali, huduma za kifedha, kazi za ofisini, burudani na upatikanaji wa taarifa kwa wakati.

Ziara hiyo imeonyesha kuwa intaneti ya kasi si huduma ya burudani pekee, bali ni nyenzo muhimu ya maendeleo inayowawezesha wanafunzi kujifunza, wafanyabiashara kufikia masoko mapya, wafanyakazi kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na familia kuwasiliana kwa urahisi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kinondoni Jogging Association, Bi. Kulusum Mpallu, amesema huduma ya Faiba Mlangoni Kwako inasogeza maisha ya kisasa karibu zaidi na wananchi kwa kuwawezesha kutumia teknolojia katika shughuli zao za kila siku.

Bi. Mpallu ameipongeza TTCL kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya mawasiliano na kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti ya kasi nchini.

Amesema uwekezaji huo una mchango mkubwa katika kuifanya Tanzania kuwa taifa la kidijitali zaidi, kuongeza fursa za ajira na biashara, kurahisisha utoaji wa huduma na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali.

Kwa upande wao, wanachama wa KIJA wameeleza kufurahishwa na maarifa waliyopata katika Kituo cha Kidigitali Kijitonyama, wakibainisha kuwa ziara hiyo imewasaidia kuelewa kwa undani zaidi nafasi ya teknolojia katika kuboresha afya, elimu, biashara, mawasiliano na ustawi wa jamii.

Pamoja na kujihusisha na shughuli za mazoezi na kuhamasisha maisha yenye afya, KIJA imeendelea kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii na kielimu zinazolenga kuwaongezea wanachama wake maarifa kuhusu fursa zinazopatikana katika jamii.

Ziara hiyo imelenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa intaneti ya kasi katika kuharakisha maendeleo ya kidijitali nchini, sambamba na kuwahamasisha wananchi kutumia huduma ya Faiba Mlangoni Kwako ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na teknolojia.

Kupitia huduma hiyo, wananchi wanaweza kutumia intaneti kwa ufanisi zaidi majumbani, katika taasisi na kwenye biashara, hivyo kuongeza tija, kuboresha mawasiliano na kufungua milango ya fursa mpya katika dunia ya kidijitali.