info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

MAWASILIANO NI BIASHARA ONGEZENI UBUNIFU-NAIBU KATIBU MKUU SMZ

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limeshauriwa kufanya kazi kwa bidii, uadilifu, kutafuta wateja na kubuni bidhaa zinazokidhi matarajio ya wateja ili waweze kuhimili ushindani wa soko la mawasiliano nchini. 

Hayo yameelezwana Naibu Katibu Mkuu Wiara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Shomari Omar Shomari wakati akifunga Kikao Kazi cha Bodi ya Wakurugenzi na Menejmenti ya shirika hilo katika hoteli ya Golden Tulip Zanzibar.

Alibainisha kwamba soko la mawasiliano kwa sasa linachangamoto nyingi ambapo kila mmoja kwenye soko hilo anabuni mkakati, teknolojia na bidhaa zenye kulenga kupata wateja wapya na kupanua wigo wa biashara kwa kila hali.

Naibu Shomari alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imewapa dhamana kubwa ya kusimamia miundombinu ya mawasiliano na wamebeba maono makubwa ya Serikali ya kuifikisha Tanzania ya Kidigitali yanafikiwa na yanaleta matunda kwa nchi.

“Nendeni mkafanye kazi kwa bidii, weledi na kwa kutanguliza uzalendo, Tanzania ya Kidigitali iko mikononi mwenu,” alibainisha. 

Aidha Naibu Shomari alisema kuwa mkutano huo ni muhimu katika kupelekea mustakabali mzuri wa Shirika hilo ikizingatia  mabadiliko ya kibiashara (business transformation) ili kukidhi mahitaji ya jamii ambapo mawasiliano yamekuwa si anasa bali nyenzo muhimu ya kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwemo elimu mtandao, afya mtandao na huduma za kifedha kupitia simu za mkononi.

Hivyo alisema ni imani yake kwamba kikao hicho kitaongeza maarifa na uelewa wa mambo mbalimbali ya kimkakati, kisheria na kisera vitakavyokuwa nguzo muhimu na msaada mkubwa wakati wa utekelezaji wa majukumu yao kama Viongozi na Wasimamizi wa shirika ili liweze kusonga mbele.

Aliipongeza Bodi na Menejimenti nzima kwa kazi nzuri wanayoifanya kwani wamekuwa mstari wa mbele kusimamia na kuendesha miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano na kusaidia kuimarika kwa mawasiliano nchini.

“Mikakati mbalimbali ambayo imetekelezwa katika kipindi hiki imesaidia kuimarisha biashara, kuinua uchumi na kuimarisha hali ya usalama wa nchi  yetu na hii inanipa imani kubwa kwamba  Mwenyekiti na Menejimenti mtafanya kazi usiku na mchana kuhakikisha matarajio ya serikali yetu kuliona shirika hili linakuwa nyenzo muhimu ya katika kuifikia Tanzania ya Kidigitali mnayanafikia kikamilifu,” alisema.

Sambamba na hayo alisema ni imani ya serikali kwamba viongozi waliopewa dhamana ya kulisimamia shirika hilo watahakikisha wanafanya kazi kwa tija na ufanisi ili liweze kuleta mageuzi makubwa katika kuimarisha Mawasiliano katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

“Tunarajiia kuona mabadiliko makubwa katika kukamilisha miradi ya mawasiliano nchini ikiwa ni pamoja na kuziunganisha Wilaya na mikoa katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ili wananchi waweze kuhudumiwa kwa haraka na ufanisi zaidi,” alisisitiza. 

 

.