MEI MOSI 2026:RAIS SAMIA AHIMIZA BIDII, UAMINIFU NA WELEDI KATIKA KUCHOCHEA UJENZI WA UCHUMI NCHINI.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan amewahimiza Wafanyakazi kufanya kazi kwa bidii, uaminifu na weledi mkubwa ili kuchochea ujenzi wa uchumi imara,maendeleo ya jamii kwa kuzingatia misingi ya Amani na Mshikamano.
Rais Samia ametoa rai hiyo wakati akihutubia Wafanyakazi katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani ‘Mei Mosi 2026’ Kitaifa yaliyofanyika Mkoani Njombe tarehe 1 Mei 2026.
Amesisitiza kuwa Serikali inathamini mchango wa wafanyakazi na itaendelea kuwaunga mkono katika juhudi za maendeleo ya nchi.Hivyo, Serikali itaendelea kuboresha maslahi ya Wafanyakazi kadiri ya uchumi unavyokuwa huku akisisitiza kufanya kazi kwa bidii.
Aidha ametoa wito kwa sekta binafsi na umma kuwekeza katika elimu na mafunzo ya ujuzi ili kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la sasa na la badaaye.
"Ajira za kesho zinahitaji ujuzi wa juu zaidi,matumizi ya teknolojia na ubunifu.Hatuwezi kuendelea na mfumo wa zamani wa uzalishaje."amesema.
Sambamba na hilo Rais Samia amesema hakuna kazi za staha bila kuwa na amani na utulivu hivyo amewataka wananchi kulinda misingi hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.
Katika maadhimisho hayo, TTCL imewakilishwa na Mfanyakazi wake Hodari Tanzania Bara ,Wafanyakazi wengine kutoka Makao makuu , Iringa na Njombe.
Ushiriki wa TTCL umeonesha dhamira yao katika kuendelea kutoa huduma bora za mawasiliano kwa wananchi,kukuza uchumi wa kidijitali na kuchangia maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Kauli mbiu ya Maadhimisho ya Mei Mosi 2026 ‘Kazi zenye Staha ni Nguzo Imara kwa Maendeleo Endelevu katika Utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050'