MHE. HALIMA DENDEGO AHAMASISHA MATUMIZI YA HUDUMA ZA TTCL
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amewahimiza wananchi, taasisi za umma na binafsi pamoja na wafanyabiashara kuendelea kutumia huduma zinazotolewa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), akieleza kuwa Shirika hilo lina mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya mawasiliano na kuharakisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Mhe. Dendego ametoa rai hiyo baada ya kutembelea banda la TTCL katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.
Akiwa katika banda hilo, alipata maelezo kuhusu huduma na miradi mbalimbali inayotekelezwa na TTCL, ikiwemo huduma ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) inayowawezesha wananchi, taasisi na wafanyabiashara kupata huduma ya intaneti ya kasi na uhakika moja kwa moja katika makazi na maeneo yao ya kazi.
Akizungumza baada ya kupata maelezo kuhusu huduma zinazotolewa na TTCL, Mhe. Dendego amepongeza juhudi za Shirika hilo katika kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu ya mawasiliano na kusogeza huduma za kidijitali karibu na wananchi.
"Huduma za TTCL zina mchango mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Nawahimiza wananchi na taasisi kuzitumia huduma hizi, hususan Faiba Mlangoni Kwako, ambayo inarahisisha upatikanaji wa intaneti ya kasi na kuunga mkono matumizi ya teknolojia katika shughuli za kila siku," amesema Mhe. Dendego.
TTCL inaendelea kushiriki katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kutoa elimu kuhusu huduma zake mbalimbali, zikiwemo Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), simu ya mkononi, T-PESA, huduma za intaneti kwa taasisi na mashirika, pamoja na suluhisho nyingine za kidijitali, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Shirika ya kuendelea kuwa kinara katika utoaji wa huduma za mawasiliano na kuchangia maendeleo ya Tanzania ya kidijitali.