info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

Miaka 60 ya Mapinduzi Zanzibar

Ukosefu wa huduma za kijamii kama maji, umeme, elimu, miundombinu pamoja na mawasiliano kwa kundi kubwa la Wazanzibari wakati wa utawala wa wakoloni ni miongoni mwa sababu ziliyopelekea kufanyika kwa mapinduzi ambayo tunayaadhimisha kwa mwaka wa 60 sasa.

Pamoja na mambo mengine ni wazi kuwa mawasiliano ni kiungo muhimu katika kuchochea maendeleo na ndiyo maana Serikali kwa kipindi chote hiki cha miaka 60 imekuwa ikijidhatiti kuimarisha mawasiliano wa Tanzania Bara na Visiwani.

Serikali kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania limeendelea kuhakikisha linaimarisha miundo mbinu ya mawasiliano ili kuwapa wananchi fursa mbalimbali ikiwemo kupata huduma za maji, umeme, afya na kuufanya mzunguko wa fedha kuwa mwepesi ikilinganishwa na hapo awali.

Katika kuhakikisha mawasiliano yanaimarika TTCL ilipeleka huduma ya mawasiliano ya 4G LTE ili kuendandana na ukuaji na mahitaji ya teknolojia ya mawasiliano na kuwapa wananchi wa Zanzibar uwezo wa kuwasiliana kwa kasi zaidi.

Uwepo wa teknolojia hii umewarahisishia wananchi wa Zanzibar mawasiliano katika shughuli zao za kila siku ikiwemo kilimo, biashara, ufugaji, pamoja na wafanyakazi wa umma na sekta binafsi.

Kuanza kutumika kwa teknolojia hii ya 4GLTE yenye gharama nafuu na uhakika, kumewezesha na kuwaunganisha wananchi katika maeneo mbalimbali kimawasiliano kwani kupitia mawasiliano biashara ya vikundi na mtu mmoja mmoja imekuwa kwa kiasi kikubwa.

Aidha katika kurahisisha zaidi shughuli za kijamii na kiuchumi TTCL kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeviunganisha visiwa vya Pemba na Unguja kwa njia ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Kuunganishwa kwa visiwa hivi ni moja ya mafanikio makubwa ya mapinduzi ya kiuchumi kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwani kuunganishwa kwa serikali hizi mbili kumewezesha gharama za mawasiliano kupungua kwa kiasi kikubwa.

Ufunguzi wa njia za mawasiliano ya Mkongo kati ya Tanzania Bara na Zanzibar una manufaa makubwa sana kwa Taifa hasa katika kuwezesha matumizi ya intaneti ambapo itakuza na kuongeza huduma za mawasiliano, kuondoa changamoto iliyokuwepo Zanzibar ya kutumia njia ya mawasiliano ya mawimbi ya radio katika kutoa huduma za mawasiliano na kupunguza gharama za mawasiliano na kuingizia Serikali mapato.

Aidha katika kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanafurahia matunda ya mapinduzi, TTCL kupitia Kampuni yake Tanzu ya T-PESA iliona ni vyema kuweka ushirikiano na Mmalaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) ili kumwezesha Mteja wa ZAWA anaondokana na adha ya kupanga foleni kulipia huduma ya maji na kumfanya kulipia huduma hiyo moja kwa moja kiganjani kwake popote atakapokuwa.

Huduma hii ya ZAWA kiganjani mwako imekuwa mkombozi mkubwa na kuleta mapinduzi chanya katika suala zima la ukusanyaji wa mapato ya serikali na hivyo kuiwezesha serikali kufanya shughuli za maendeleo kwa wananchi wake.

Makubaliano haya kati ya TTCL na Mamlaka ya Maji Zanzibar yamesaidia kwa kiwango kikubwa kuondoa utapeli ambao wananchi walikuwa wanafanyiwa na watu ambao si waaminifu lakini pia imeondoa uwezekano wa viashiria vya rushwa baina ya mteja na mtoa huduma na kufuta upendeleo katika kutoaji huduma ambayo yote yalichagizwa na uwepo wa foleni za kusubiri huduma kwa muda mrefu.

TTCL itaendelea kutoa huduma bora za Mawasiliano na usimamizi wa Miundombinu ya Kimkakati ya Mawasiliano Nchini na kutoa ajira kwa kuzingatia pande zote za Muungano hali ambayo imezidi kuimarisha na kustawisha ushirikiano, udugu na uhusiano mwema.

Katika hatua nyingine TTCL imekuwa ikitimiza vyema majukumu yake katika Ofisi zake zote Tanzania Visiwani ambapo inahudumia Serikali, Taasisi za Umma na Sekta binafsi chini ya ushirikiano mzuri wa Viongozi Wakuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 

Moja ya sekta hizo ni sekta ya huduma za fedha ambapo T-Pesa katika kuhakikisha inafikisha huduma kwa wananchi kwa wakati na gharama nafuu iliingia makubaliano ya kibiashara na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) ili kuwawezesha mawakala wa T-Pesa kuhudumiwa na PBZ bila makato ya ziada.

Hii ni kuweka urahisi na unafuu wa gharama na kuwawezesha mawakala kutoa huduma stahiki kwa wateja wa T-Pesa na kujipatia kipato kwa ajili ya ustawi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.

Benki ya PBZ ni moja ya taasisi za fedha kongwe ambayo inailikiwa kwa asilimia 100 na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hivyo T-Pesa kuingia makubaliano na Benki hiyo kumewezesha huduma ya fedha mtandao kuenea kwa kasi kubwa ikizingatiwa kuwa PBZ ni taasisi kubwa ya kifedha inayotoa huduma Zanzibar, Pemba na Tanzania Bara kwa ujumla.

Pamoja na kwamba mawakala wa T-Pesa wanapata huduma za kifedha kupitia PBZ pia PBZ inatumia huduma zingine za TTCL kama huduma za simu na vifurushi pamoja na data katika kuendesha shughuli zake za kila siku na hivyo mapato yatokanayo na huduma hizi kusaidia kuleta maendeleo katika serikali hizi mbili.

Kwa TTCL miaka 60 ya Mapinduzi Matukufu imeleta ufanisi mkubwa katika utendaji wa shughuli za serikali hasa katika maeneo ya Elimu, Afya, kilimo mtandao na kukidhi matarajio ya Serikali ya kuziba pengo la matumizi ya Tehama kwa wananchi katika kuwapatia huduma kwa haraka zaidi.

Pia imeboresha huduma za mawasiliano ya sauti na data na hivyo kurahisisha maendeleo kiuchumi, kijamii vilevile kuimarisha usalama wa nchi kupitia huduma ya teknolojia ya mawasiliano.

.