MKURUGENZI MKUU TTCL AWAKARIBISHA WANANCHI KUJIONEA SULUHISHO ZA KIDIJITALI SABASABA 2026
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) Moremi Marwa amewaalika wananchi kutembelea Banda la TTCL katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) ili kujionea mageuzi ya kiteknolojia na suluhisho mbalimbali za kidijitali zinazotolewa na Shirika katika kuimarisha huduma za mawasiliano na kuchochea uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumza alipotembelea banda la TTCL katika Viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere, Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu alisema ushiriki wa TTCL katika maonesho hayo unalenga kuwaonesha wananchi maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano pamoja na bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika kupitia miundombinu ya kisasa ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB).
Alieleza kuwa huduma nyingi za kidijitali zinazotolewa na TTCL zinategemea Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao umeendelea kuwa nguzo muhimu katika kuunganisha taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi, huku ukiwezesha upatikanaji wa intaneti ya kasi ya juu na kuimarisha maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
"Maonesho haya yanatupa fursa ya kuwaonesha wananchi uwezo wa TTCL katika kutoa suluhisho za kisasa za mawasiliano na kuwafahamisha namna teknolojia inavyorahisisha maisha ya kila siku na shughuli za kiuchumi," alisema.
Miongoni mwa vivutio vinavyopatikana katika Banda la TTCL ni FTTX Experience Centre, eneo linalowawezesha wananchi kujionea matumizi ya teknolojia ya intaneti ya nyuzi macho (fiber optic) katika kuendesha nyumba mahiri (Smart Home). Kupitia teknolojia hiyo, vifaa mbalimbali vya nyumbani kama taa, televisheni, friji, jiko na mifumo ya ulinzi vinaweza kuunganishwa na kudhibitiwa kwa njia ya mtandao.
Aidha, TTCL inaendelea kutambulisha huduma za Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data (National Internet Data Centre – NIDC), kinachotoa suluhisho za Cloud Computing kwa taasisi na wateja binafsi wanaohitaji kuhifadhi na kusimamia taarifa zao kwa usalama bila kuwekeza katika miundombinu mikubwa ya TEHAMA.
Mkurugenzi Mkuu alisisitiza kuwa huduma hizo zote zinawezeshwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, ambao unaendelea kupanua upatikanaji wa intaneti ya kasi nchini na kuweka msingi imara wa utoaji wa huduma za kidijitali katika sekta mbalimbali za uchumi.
Aliongeza kuwa mageuzi yaliyotekelezwa ndani ya TTCL kwa maelekezo ya Serikali yameimarisha uwezo wa Shirika kujiendesha kibiashara, kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma na kuendelea kuwekeza katika teknolojia za kisasa zinazokidhi mahitaji ya wananchi na taasisi.
Mkurugenzi Mkuu amewahimiza wananchi, taasisi za umma na sekta binafsi kutembelea Banda la TTCL katika Maonesho ya Sabasaba 2026 ili kujionea suluhisho mbalimbali za kidijitali, kupata elimu kuhusu huduma zinazotolewa na Shirika pamoja na kunufaika na ofa maalum zinazotolewa katika kipindi chote cha maonesho.