MKURUGENZI MKUU WA TTCL AFANYA ZIARA KATIKA BANDA LA TTCL MAONESHO YA 49 YA SABASABA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation, Bw. Moremi Marwa, leo Julai 4, amefanya ziara maalum katika Banda la TTCL lililopo kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa (SabaSaba), yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo, Bw. Marwa alipokelewa na wataalamu waandamizi kutoka TTCL ambao walimpitisha katika maeneo mbalimbali ya banda hilo na kumuelezea kwa kina huduma na teknolojia zinazotolewa na Shirika hilo.
Akiwa katika banda hilo, wataalamu wa TTCL walimweleza Mkurugenzi Mkuu kuhusu huduma ya Faiba Mlangoni, ambayo inapeleka intaneti ya kasi moja kwa moja kwa wateja majumbani na maofisini ikiwa ni sehemu ya jitihada za Shirika hilo kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora ya mawasiliano kwa gharama nafuu.
Aidha, alielezwa kwa kina kuhusu Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) miundombinu muhimu ya kimkakati ikiwa umesamnbazwa katika mikoa yote 26 na wilaya 112 kati ya 139 nchi nzima ha kuziunganisha inchi jirani na hivyo kuwa kichocheo cha ukuaji wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa Wananchi.
Pia alielezwa kuhusu Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) ambacho kimejengwa kwa teknolojia ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhi na kulinda taarifa muhimu za taasisi, makampuni na taasisi za kimataifa na hivyo kuchangia ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Wataalamu walieleza pia kuhusu huduma ya Call Center ambayo ni suluhisho la kimawasiliano linalosaidia mashirika kuwasiliana na wateja wao kwa njia ya kitaalamu, pamoja na huduma ya WiFi ya Umma (Public WiFi) inayowezesha wananchi kupata intaneti katika maeneo ya wazi kwa urahisi zaidi.
Aidha Mkurugenzi Mkuu alipata fursa ya kutembelea mabanda ya taasisi nyingine ambayo ni POSTA, UCSAF, TCRA, SIDO, TIRA pamoja na banda la Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari huku akifuatana na maafisa waandamizi wa TTCL.
Ziara hii ililenga kuimarisha ushirikiano baina ya taasisi hizi katika kuhakikisha Watanzania wananufaika na mapinduzi ya kidijitali na maendeleo ya sekta ya mawasiliano nchini.