MKURUGENZI MKUU WA TTCL AKAGUA MIRADI YA KIMKAKATI YA MAWASILIANO KIGOMA, KUIMARISHA UUNGANISHAJI WA KIKANDA NA UKUAJI WA BIASHARA
Na Godfrey Andafiche
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, amefanya ziara mkoani Kigoma kwa lengo la kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya mawasiliano, inayolenga kuimarisha miundombinu ya kidijitali, kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kufungua fursa mpya za biashara ndani na nje ya Tanzania.
Miongoni mwa miradi iliyokaguliwa ni ujenzi wa kituo cha makutano ya mkongo wa mawasiliano kutoka Ziwa Tanganyika kwenda nchi kavu, ambao ni sehemu ya mpango wa TTCL wa kuimarisha muunganisho wa mawasiliano kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kupitia Kigoma.
Mradi huo wa kimkakati umelenga katika kuongeza uwezo na upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika ukanda wa Ziwa Tanganyika, huku ukiweka msingi wa Tanzania kushiriki kikamilifu katika kukuza uchumi wa kidijitali na biashara za kidijitali zinazovuka mipaka.
Kupitia miundombinu hiyo, TTCL inalenga kuchangia upatikanaji wa mawasiliano yenye uwezo mkubwa na yanayoaminika, sambamba na kuwezesha taasisi, wafanyabiashara na wananchi kunufaika na fursa zinazotokana na uchumi wa kidijitali.
Katika ziara hiyo, Mkurugenzi Mkuu pia alikagua maeneo yanayohusishwa na utekelezaji wa Faiba Mlangoni (FTTH) Phase II, mradi unaolenga kusogeza huduma za intaneti ya kasi moja kwa moja hadi kwa wateja katika maeneo ya makazi na biashara.
Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika kata nne za Manispaa ya Kigoma, na ni sehemu ya juhudi za TTCL kupanua huduma za intaneti ya kasi na kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali kwa wananchi, taasisi na wafanyabiashara.
Aidha, Mkurugenzi Mkuu alitembelea mnara wa mawasiliano uliopo Maragarasi, unaotoa huduma kwa wananchi wa vijiji vinavyouzunguka pamoja na kuwezesha mawasiliano katika eneo la utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa bwawa la kufua umeme.
Akiwa katika eneo hilo, Bw. Marwa alielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Ufundi kuchukua hatua stahiki za kuboresha na kuimarisha ubora wa huduma za mawasiliano, ili kuhakikisha wananchi na wadau wanaotekeleza miradi ya maendeleo wanapata huduma za mawasiliano zenye ufanisi na zinazoendana na mahitaji ya eneo.
Akizungumza kuhusu umuhimu wa miradi hiyo, Mkurugenzi Mkuu alisisitiza kuwa uwekezaji katika miundombinu ya mawasiliano ni sehemu muhimu ya mkakati wa TTCL wa kupanua wigo wa biashara, kuongeza thamani kwa wateja na kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali.
Kwa kuimarisha miundombinu kutoka Tanzania kuelekea masoko ya kikanda, sambamba na kusogeza huduma za intaneti kwa kasi kwa wananchi na wafanyabiashara, TTCL inaendelea kujenga msingi wa Tanzania iliyounganishwa zaidi, yenye uchumi wa kidijitali unaokua na fursa pana zaidi za biashara na uwekezaji.
Ziara hiyo ni sehemu ya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya TTCL na kuhakikisha uwekezaji wa Shirika unazalisha thamani kwa wateja, wananchi, Serikali na wadau wengine.