info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

N-CARD SASA KUWA JAMII KADI

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry Silaa ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa Kituo cha Kitaifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC) wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), alipotembelea kituo hicho kukagua utendaji kazi wa mradi wa N-CARD.

Akiwa pamoja na Waziri Mkuu, Mhe. Silaa aliviambia vyombo vya habari kuwa mradi wa N-CARD ni hatua kubwa katika mageuzi ya kidijitali nchini, ambapo Serikali inaendelea na mchakato wa kurahisisha malipo kwa kutumia kadi moja ya itakayoitwa Jamii Kadi ambayo itawaunganisha wananchi na huduma za kijamii, kifedha, afya, elimu na nyingine nyingi kupitia utambulisho mmoja wa kidijitali.

 “N-CARD ‘Jamii Kadi’ itakuwa chombo muhimu cha kuwezesha upatikanaji wa huduma za umma na binafsi kwa njia ya kisasa, ni hatua muhimu kuelekea Tanzania ya kidijitali ambapo wananchi wataweza kufanya malipo mbalimbali ikiwemo viingilio vya viwanja vya michezo, malipo ya vivuko, huduma ya ukataji tiketi katika Standi Kuu za Mabasi na katika Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (UDART),” alisema Mhe. Silaa.

Katika hatua nyingine Waziri Silaa alizihimiza Taasisi za Umma na Sekta Binafsi na Kampuni mbalimbali kuwekeza na kutumia huduma zinazotolewa na NIDC kwani Kituo hicho si tu kinatoa huduma za kuhifadhi data kwa usalama mkubwa, bali pia kinatoa majukwaa ya TEHAMA kwa bei nafuu ambayo yatasaidia taasisi hizo kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza ufanisi.

“Tunatoa wito kwa Mashirika, Taasisi za serikali na sekta binafsi kutumia NIDC kwa ajili ya kuhifadhi data zao, …hiki ni kituo chetu cha Taifa, chenye viwango vya kimataifa, na ni mali ya Watanzania wote,” aliongeza Waziri Silaa.

Alisema juhudi hizi za kuendeleza NIDC na mradi wa N-CARD, ni dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb), katika Kituo cha Kuhifadhi Data Kimtandao (National Internet Data Centre – NIDC), kinachomilikiwa na kusimamiwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL, alioneshwa mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia uwekezaji wa serikali katika sekta ya TEHAMA ambapo TTCL ina jukumu la kuhakikisha usalama na uhifadhi wa taarifa za kimkakati za taasisi za serikali na sekta binafsi huku NIDC ikiwa ni kiini cha mapinduzi ya kidigitali hapa nchini ikitoa huduma za kuhifadhi data, miundombinu ya kimtandao na kuwa suluhisho la TEHAMA.

Kupitia kituo hiki, Tanzania inazidi kujihakikishia uhuru wa kidigitali, uthabiti wa mifumo ya serikali, na mazingira salama ya kuhifadhi taarifa ikiwa ni utekelezaji wa azma ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kidigitali.

.