info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

NICTBB NA ESCOM KULETA MABADILIKO SEKTA YA MAWASILIANO

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania-TTCL kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) limesaini Mkataba wa Makubaliano ya Kibiashara na Kampuni ya Serikali ya Malawi inayosimamia Mkongo wa Mawasiliano - Electricity Supply Corporation of Malawi Limited (ESCOM). 

Makubaliano haya ya Kibiashara yamesainiwa Septemba 8 mwaka huu kati ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL Mhandisi Peter Ulanga na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Serikali ya Malawi inayosimamia Mkongo wa Mawasiliano (ESCOM) Bw. Kamkwamba Kumwenda.

Hafla hiyo ya kusaini Makubaliano hayo ilifanyika Zanzibar na kushuhudiwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe Nape Nnauye (Mb), Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe Khalid S. Mohamed na Waziri anayesimamia Mawasiliano kutoka Serikali ya Malawi (Ministry of Information and Digitalisation), Mhe. Moses Kunkuyu Kalongashawa.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Mhandisi Ulanga alisema Makubaliano hayo yatakuwa chachu katika kuleta mageuzi ya kimaendeleo katika sekta mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kijamii na kiusalama. 

Aidha alisema TTCL kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano – NICTBB ipo tayari kuhakikisha inatoa huduma inayostahili kwa Malawi kwa kuzingatia masharti yaliyopo katika Mkataba huo.

Naye Mtendaji Mkuu wa ESCOM Bw. Kamkwamba Kumwenda alisema matarajio yao makubwa ni kupata huduma bora za mawasiliano ambayo yataleta mabadiliko  kwa Wananchi wa Malawi ambayo yatawezesha ukuaji wa uchumi kupitia sekta ya biashara na sekta zingine nchini humo.

Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano- NICTBB na Mkongo wa Taifa wa Malawi –ESCOM zimeunganishwa kupitia eneo la Kasumulo mpaka wa Tanzania na Malawi, katika Wilaya ya Kyeka mkoani Mbeya.

 

.