POLISI DAR ES SALAAM YAWAKAMATA 11 KWA TUHUMA ZA HUJUMA MIUNDOMBINU YA TTCL
Na Adeline Berchimance
Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam limewakamata watu 11 wanaodaiwa kujihusisha na wizi, uharibifu, usafirishaji na biashara ya miundombinu ya mawasiliano ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), huku likisema hali ya usalama jijini kwa ujumla ni shwari.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Agosti 27, 2026, katika Ukumbi wa Mikutano wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro, amesema operesheni hiyo imefanyika kwa ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi na Kitengo cha Usalama cha TTCL baada ya kubaini matukio ya hujuma dhidi ya miundombinu ya mawasiliano.
Kamanda Mliro amesema uchunguzi na ufuatiliaji wa mtandao huo umefanyika kwa kipindi cha miezi mitatu, kuanzia Juni hadi Agosti 2026, huku vikosi na vitengo mbalimbali vya Jeshi la Polisi vikishirikishwa, ikiwemo Kamisheni ya Upelelezi na Polisi Jamii,
“Katika operesheni hizi tumefanikiwa kuwakamata watu 11 wanaotuhumiwa kupanga, kuharibu, kuiba, kusafirisha na kufanya biashara ya miundombinu ya mawasiliano ya TTCL,” amesema Kamanda Mliro.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, watuhumiwa hao walikuwa wakilenga zaidi nyaya za mawasiliano zinazobeba huduma muhimu zinazotumiwa na taasisi mbalimbali za Serikali na zisizo za Serikali.
Uharibifu wa miundombinu hiyo, amesema, unaweza kuvuruga huduma za mawasiliano zinazowezesha shughuli za kiuchumi, kijamii na kiutawala.
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi ya watuhumiwa walikuwa wakitumia zana mbalimbali, ikiwemo nyundo, sururu, majembe na misumeno, kuchimba, kukata na kuondoa miundombinu hiyo.
Aidha, baadhi yao walidaiwa kujifanya kuwa wafanyakazi au wakandarasi wanaofanya shughuli za matengenezo, kwa kuvaa mavazi yanayofanana na ya wafanyakazi wa miundombinu, yakiwemo kofia ngumu, reflective jackets, buti na gloves, ili kurahisisha utekelezaji wa vitendo hivyo bila kuzua shaka.
Kamanda Mliro amesema Jeshi la Polisi linachukulia vitendo hivyo kwa uzito mkubwa kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kwa huduma za mawasiliano na shughuli zinazotegemea miundombinu hiyo.
Jeshi hilo limetoa onyo kwa mtu, kundi au mtandao wowote unaojihusisha na kupanga, kuiba, kuharibu, kusafirisha au kupokea miundombinu ya mawasiliano kwa ajili ya biashara, likisisitiza kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wote watakaobainika kuhusika.
Wakati huo huo, Kamanda Mliro amewataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za kweli kuhusu vitendo vya uhalifu, akisisitiza kuwa taarifa zinazotolewa kwa vyombo vya usalama zitalindwa kwa kuzingatia usiri.
Amesema ushirikiano wa wananchi umekuwa muhimu katika kufanikisha operesheni mbalimbali za kupambana na uhalifu, pamoja na makosa yanayohusiana na usalama barabarani.
Katika hatua nyingine, Kamanda Mliro amesema hali ya usalama jijini Dar es Salaam kwa ujumla ni shwari, huku shughuli za kisiasa, kiuchumi na kijamii zikiendelea bila changamoto kubwa za kiusalama.
Amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam litaendelea kushirikiana na wadau, wakiwemo TTCL, katika kulinda watu, mali na miundombinu muhimu ya taifa, pamoja na kuhakikisha sheria inazingatiwa.