RAIS MWINYI ATEMBELEA BANDA LA TTCL KIZIMKAZI.
Na Adeline Berchimance
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametembelea Banda la Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika Maonesho ya Tamasha la Kizimkazi 2026, ambapo amepata fursa ya kufahamu huduma na mchango wa TTCL katika kuimarisha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Mhe. Dkt. Mwinyi amepokelewa na Meneja wa TTCL Zanzibar, Bi. Nasra Mugheiry , ambaye amemueleza kuhusu shughuli zinazotekelezwa na Shirika katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za mawasiliano zenye ubora, uhakika na zinazokidhi mahitaji ya zama za kidijitali.
Katika maelezo yake, Bi. Mugheiry ameeleza kuwa TTCL imeendelea kusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar, hatua inayosaidia kuimarisha upatikanaji wa huduma za intaneti na kuwezesha wananchi, taasisi na wafanyabiashara kunufaika na fursa zinazotokana na teknolojia ya kidijitali.
Ameeleza pia kuwa uwekezaji huo umewezesha wananchi wengi kupata huduma ya FTTH (Fiber To The Home), inayowapatia intaneti ya kasi majumbani kwa gharama nafuu.
Amesema Huduma hiyo imekuwa muhimu kwa familia, wanafunzi, wafanyabiashara na wataalamu wanaotegemea intaneti katika elimu, biashara, mawasiliano na kazi za kila siku.
Katika ziara hiyo, Rais Mwinyi pia amefahamishwa kuhusu nafasi ya National Internet Data Centre (NIDC) katika kuwezesha uchumi wa kidijitali kupitia huduma za kisasa za miundombinu ya TEHAMA.
Ameelezwa huduma zinazotolewa na NIDC, ikiwemo Cloud Computing, Colocation na Virtual Server, kwamba zinawezesha taasisi na wafanyabiashara kupata miundombinu ya TEHAMA yenye uhakika kwa ajili ya kuhifadhi, kuendesha na kusimamia mifumo na taarifa zao.
Huduma hizi zina umuhimu mkubwa katika safari ya Tanzania kuelekea uchumi unaotegemea teknolojia, kwani zinasaidia taasisi kupunguza gharama za uwekezaji katika miundombinu ya TEHAMA, kuongeza ufanisi na kuwezesha upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa urahisi na usalama zaidi.
Uwekezaji katika Mkongo wa Taifa, huduma za intaneti ya kasi kupitia FTTH pamoja na huduma za NIDC unaendelea kuiweka TTCL katika nafasi muhimu ya kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, hususan katika kujenga uchumi shindani unaotumia teknolojia na ubunifu.
Ziara ya Rais Dkt. Mwinyi katika Banda la TTCL pia imekuwa fursa muhimu kwa Shirika kuonesha kwa vitendo huduma na teknolojia zinazotolewa, pamoja na namna TTCL inavyoendelea kuwa sehemu ya safari ya Tanzania kuelekea Taifa la kidijitali.
Tamasha la Kizimkazi 2026 linafanyika Kizimkazi, Zanzibar, likiwa na kaulimbiu “Kizimkazi Kumenoga – Shangwe na Fursa,” huku TTCL ikiwa miongoni mwa washiriki na wadau wanaounga mkono tamasha hilo.