info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

SERIKALI ITAENDELEA KUHUISHA VIWANGO VYA MSHAHARA- DKT. MPANGO

Wafanyakazi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL Corporation wameungana na Wafanyakazi wenzao duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu Mei Mosi ambayo huadhimishwa kila tarehe Moja ya Mwezi wa Tano kila mwaka.

Nchini Tanzania maadhimisho hayo yalifanyika Kitaifa katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid Mkoani Arusha yakiwa na Kauli Mbiu ya "Nyongeza ya Mishahara ni msingi wa Mafao Bora na Kinga dhidi ya Hali ngumu ya Maisha" huku Mgeni rasmi akiwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango.

Akizungumza katika maadhimisho hayo Mhe. Dkt. Mpango alikiri wazi mbele ya Wafanyakazi kwamba anatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na wafanyakazi wote nchini katika kuhakikisha Tanzania inasonga mbele kiuchumi na kuwapongeza kwa kazi hiyo na kuwataka kuendelea kuchapa kazi kwa bidii ili kuliwezesha Taifa hili kufika mbali zaidi.

Akiizungumzia kauli mbiu ya mwaka huu Dakta Mpango alisema Serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mshahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa waajiriwa ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la Taifa na athari nyingine kwenye utulivu wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Aidha alisema changamoto mbalimbali ambazo zimeikumba Dunia ikiwemo vita na majanga ya asili zimeendela kuathiri uchumi wa Taifa kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa ugavi na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea, chuma na chakula.

Mhe. Dkt. Mpango alisema pamoja na changamoto hizo tathmini ya Serikali na ya Taasisi za Kimataifa ikiwemo IMF, Benki ya Dunia, AfDB, Moody’s, Fitch na zinginezo zimeonesha kuwa uchumi wa Taifa umekuwa stahimilivu kwa kiasi cha kuridhisha hivyo hali hiyo itakapoendelea kudumu wafanyakazi wawe tayari kunufaika.

Hata hivyo aliwataka Wafanyakazi wote nchini kuendeleakuchapa kazi na  kutekeleza majukumu yao kwa bidii, uadilifu na maarifa huku wakitanguliza maslahi ya Taifa ili kuleta tija na ufanisi katika ukuaji wa uchumi. Aidha alivisihi Vyama vya Wafanyakazi kushirikiana na Serikali na Waajiri kuhakikisha tija inaongezwa kwenye maeneo ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.

Katika hatua nyingine Makamu wa Rais alitumia maadhimisho hayo kuzungumzia suala la Likizo ya Uzazi kuwa ni haki ya Mfanyakazi na iwapo mfanyakazi husika atajifungua mtoto au watoto Njiti, kipindi cha uangalizi maalumu hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi, na kuongeza kuwa  mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya kawaida ya uzazi ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha. 

Aliongeza kuwa Serikali ipo katika hatua ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura 366 ili likizo ya uzazi ianze pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum kadri madaktari watakavyothibitisha.

Halikadhalika aliwasisitiza na kuwaasa wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti pindi wanaponunua bidhaa na kuhakikisha risiti wanazopewa zimeandikwa gharama halisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato halisi ili kuiwezesha serikali kuwa na wigo mpana wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.

Sambamba na yote, Mhe. Dkt. Mpango alitoa tuzo mbalimbali pamoja na vyeti kwa Wafanyakazi Bora kutoka kwenye Taasisi, Mashirika na Idara mbalimbali za Serikali huku Bw. Daudi Mabula Mfanyakazi bora wa TTCL kwa mwaka 2024 akiwa ni miongoni mwa Wafanyakazi Bora waliopata fursa ya kukabidhiwa Cheti cha Pongezi kutoka kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango

Kihistoria Sikukuu ya wafanyakazi duniani ni kumbukumbu ya mauaji ya mwaka 1886 yaliyotokea katika viwanja vya Haymarket Chicago, Marekani. Mauaji haya yalifanyika katika harakati za Polisi kutawanya mkusanyiko wa Wafanyakazi walikuwa katika maandamano na mgomo wa kupinga maslahi duni na saa nyingi za kufanya kazi na hivyo kukosa muda wa kupumzika na kujumuika na jamaa zao katika jamii.

Aidha ni siku ambayo Vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi kwa ujumla huitumia kupaza sauti kuelezea changamoto wanazokabiliana nazo katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kuomba mazingira bora ya kufanyia kazi na unafuu wa gharama za maisha kwakuwataka waajiri kuwaboreshea maslahi hususani mishahara.

 

.