info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

SERIKALI NA WATOA HUDUMA ZA MAWASILIANO NCHINI WASAINISHANA MIKATABA

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari chini ya Serikali ya Tanzania imefikia makubaliano ya kihistoria na Watoa Huduma wa Mawasiliano (Consourtium of Telco-Operators) yenye thamani ya Shilingi bilioni 50 kama malipo ya matumizi ya miundombinu ya Mkongo wa Mawasiliano tangu kujengwa kwake. Hafla hiyo ilihusisha utiaji saini hati ya Maridhiano na hati ya Mkataba wa nyongeza kwenye miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. 

Hafla hiyo ilifanyika tarehe 25 Septemba 2023 katika Ukumbi wa Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam ambapo Viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu na Wakuu wa Taasisi za Huduma ya Mawasiliano nchini ikiwemo Shirika la Mawasiliano Tanzania walihudhuria.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Moses Nnauye, alisisitiza umuhimu wa kuendeleza Sekta ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano (ICT) kwa ajili ya kuifikisha Tanzania katika Uchumi wa Kidijiti kwa kuimarisha miundombinu ya Mawasiliano, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa katika maeneo ambayo hayakuwa na huduma ya Mawasiliano.

Pia Mhe. Nape Moses Nnauye, aliupongeza Umoja wa Watoa Huduma wa Mawasiliano (Consourtium of Telco-Operators) kwa kufikia muafaka wa maridhiano hayo bila ya kwenda mahakama na kusisitiza kuwa waadilifu katika kutekeleza majukumu yao kama ilivyoainishwa katika hati ya Makubaliano ili kuwafikishia Watanzania huduma bora ya Mawasiliaino. 

Pamoja na pongezi hizo Waziri Nape aliwataka watoa huduma hao za mawasiliano kuendelea kuwekeza katika miundombinu inayowezesha kufikisha kwa wananchi na kuongeza kuwa kusainiwa mikataba na hati hizo ni uthibitisho wa utayari wa serikali katika kuhakikisha inaungana na sekta binafsi ili kuleta ufanisi katika sekta ya mawasiliano nchini.

Aidha alibainisha kuwa hatua hiyo imefikiwa kufuatia nia ya dhati na maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutatuliwa kwa mgogoro uliokuwepo kati ya serikali na umoja huo jambo lililosababisha kukwama kwa shughuli za uwekezaji.

Waziri Nape alibainisha kuwa kumalizika kwa mgogoro huo uhusiano umerejea na tayari Umoja huo wa Watoa huduma za Mawasilaina nchini umeiahidi serikali kukabidhi miundombinu wa mawasiliano wenye urefu wa takribani kilomita 3000.

 

 

.