info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

T-PESA YAPATA BODI MPYA YATAKIWA KUTIMIZA MALENGO

T-Pesa ni Kampuni Tanzu ya Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL Corporation ambayo majukumu yake ni kutoa huduma ya kifedha kwa njia ya mtandao ikiwapa wigo mpana, usalama na unafuu watumiaji kutuma, kupokea, na kuhifadhi pesa kwa kutumia simu zao za mkononi.

Ili kutimiza majukumu hayo kampuni hiyo hivi karibuni imezindua Bodi mpya ya Wakurugenzi TTCL PESA LIMITED pamoja na Bodi ya Wadhamini ya TTCL Pesa Trust Entity ili kuimarisha usimamizi wa huduma hiyo ya kifedha. 

Uwepo wa Bodi ya Wakurugenzi kutachangia katika kuweka mikakati ya biashara na kufanya maamuzi muhimu kuhusu uendeshaji wa huduma ya T-Pesa, kutathimini mwenendo wa soko na kusimamia utekelezaji wa mikakati ya ukuaji wa kampuni.

Akizindua Bodi hiyo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la mawasiliano Bi. Zuhura Muro aliitaka T-PESA kuhakikisha inaongeza ubunifu wa bidhaa na huduma inazozitoa kwa wateja wake ili iweze kutimiza maono ya TTCL ikiwa ni pamoja na kutengeneza faida na kuongeza hisa. 

Alisema T-PESA ikiongeza ubunifu zaidi italisaidia Shirika kutimiza maono ya kukamilisha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano ambao unalenga kuchochea mabadiliko katika sekta ya mawasiliano hapa nchini na nje ya nchi.

Bodi ya Wakurugenzi itawakilisha maslahi ya wadau mbalimbali wa T-Pesa, ikiwa ni pamoja na wawekezaji, wateja, na jamii kwa ujumla na kuhakikisha maamuzi yanayofanywa na kampuni yanazingatia mahitaji na matarajio ya wadau wote.

Aidha itahakikisha huduma ya T-Pesa inafuata viwango vya juu vya uwazi, uwajibikaji, na maadili na kushiriki katika kuweka malengo ya muda mrefu na hivyo kuleta mafanikio ya kampuni katika sekta ya huduma za kifedha nchini.

Bodi ya TTCL PESA immejipanga vizuri ili kuhakikisha Kampuni ya T-PESA inakuza uchumi wa kidigitali na kuongeza mapato ya nchi nakuweka mikakati ya kuongeza hisa na kupanua wigo wa biashara ili kuongeza faida na kuiwezesha Serikali kupata gawio

Akizungumza mara baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya TTCL PESA, Bw. Richard Mayongela alisema Bodi imejipanga kikamilifu kutekeleza majukumu yake ili kutimiza maono ya TTCL ambayo yatasaidia katika utekelezaji wa ujenzi wa uchumi wa kidigitali nchini. 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Mhandisi Peter Ulanga alisema lengo la TTCL ni kuiona T-PESA inatoa huduma bora a fedha mtandao nchini na nje ya mipaka ya Tanzania.

Wajumbe wapya wa Bodi ya TTCL PESA na Bodi ya Wadhamini ni pamoja na Bw.Mohamed Nyengi, Dr.Maduhu S.Kazi, Bi.Agatha Keenja, Mwanahiba M. Mzee, Bw. Ansel Missango, Bi. Irene Madeje Mlola, Dkt. Maduhu I. Kazi, Bw. Salum Awadh na Bi. Mary Kinabo.