
T-PESA YATOA MWELEKEO MPYA WA UBORESHAJI WA MIAMALA YA KIDIJITALI AFRIKA
Kampuni ya huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali, T-Pesa, imeonesha dira ya maboresho ya miamala ya pesa barani Afrika kupitia wasilisho la kitaalam lililotolewa na Afisa Mipango wa Kampuni hiyo Bw. Yusuph Kalamba, wakati wa Tamasha la Teknolojia ya Fedha Afrika (Fintech Festival 2025) lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Katika wasilisho hilo Bw. Kalamba alibainisha kuwa matumizi ya teknolojia ya kisasa yanatoa fursa ya kuimarisha huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, jambo ambalo linaweza kuchochea ukuaji wa uchumi na ujumuishwaji wa kifedha barani Afrika.
Akizungumzia uboreshaji Miamala ya Pesa za Kidijitali na Malipo ya Simu ya Kielektroniki barani Afrika Kalamba alieleza kuwa bado kuna changamoto nyingi katika kufanya miamala ya kimataifa, ikiwemo tofauti za kisheria kati ya nchi na nchi, viwango vya ubadilishaji wa fedha, na ukosefu wa ulinganifu wa mifumo ya malipo kati ya mataifa.
“Changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa mfumo wa pamoja wa malipo kupitia simu za mkononi kati ya nchi mbalimbali za Afrika. Hii inasababisha mteja kutoka nchi moja kushindwa kufanya malipo ya moja kwa moja katika nchi nyingine,” alisema Kalamba.
Alitoa wito kwa nchi za Afrika kushirikiana katika kutengeneza sera na mifumo jumuishi ya malipo ya kidijitali itakayowezesha wateja kutoka mataifa tofauti kufanya miamala bila vikwazo vya kiteknolojia au kisheria.
Aliongeza kuwa suluhisho la changamoto hizi ni kuwa na mfumo wa pamoja wa malipo barani Afrika utakaorahisisha huduma kwa wateja wa kada zote – hata wale walio nje ya mfumo rasmi wa kibenki.
Tamasha hilo la Teknolojia ya Fedha linawakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya Fedha, Teknolojia, Serikali na Mashirika ya Kimataifa kujadili mustakabali wa huduma za kifedha barani Afrika, huku T-Pesa ikionekana kuwa miongoni mwa wabunifu wanaotoa mwelekeo mpya wa mageuzi ya kidijitali.