info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

TAASISI, MASHIRIKA, WIZARA TUMIENI DATA CENTRE KUTUNZA DATA KIMTANDAO – KATIBU MKUU WHMTH

Wito umetolewa kwa Taasisi, Mashirika ya Umma na binafsi na Wizara mbalimbali kutumia Kituo cha Kutunza Data Kimtandao (Data Centre) ili kutunza kumbukumbu zao kimtandao katika hali ya ubora na usalama zaidi.

Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Bw. Mohamed K. Abdullah hivi karibuni wakati wa ziara ya kikazi aliyoifanya TTCL ya kukagua vifaa vitakavyotumika katika Mradi wa Upanuzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wa Awamu ya Tatu utakahusisha Wilaya 32 nchini.

Katika ziara hiyo Bw. Abdullah alipata wasaa wa kuzungumza na vyombo vya habari ambapo alisema kituo hicho cha kuhifadhi kumbukumbu (Data Center) ni cha kisasa kina nafasi ya kutosha hivyo ni vyema Kampuni, Taasisi, Mashirika na wizara mbalimbali ambazo bado hazijaanza kutumia kituo hicho kuanza kufanya hivyo kwa ajili ya usalama wa kumbukumbu zao.

Alibainisha kuwa Kituo cha Kutunza Data Kimtandao kina miundombinu ya uhakika kwa ajili ya kutunza data kwa Wateja wa ndani na nje ya nchi na kwamba kituo hicho kimepata udhibitisho wa ubora kutoka Shirika la Viwango la Kimataifa- International Organisation of Standardisation (ISO).

Katika hatua nyingine Bw. Abdullah alilitaka Shirika la mawasiliano Tanzania kuhakikisha linakamilisha miradi ya mawasiliano kwa haraka kwakuzingatia ubora ili kuziwezesha shughuli zinazotegemea mawasiliano kufanyika kwa ufanisi na hivyo wananchi kupata huduma mbalimbali za kijamii kwa haraka na ubora Zaidi.

Bw.Abdullah alisema matarajio ya Serikali ni kuona miradi inakamilika kwa wakati na kwa ufanisi kwani TTCL sasa imewezeshwa kikamilifu, "TTCL ile ya zamani sio kama ya sasa hivi,hivyo sitarajii mtuangushe kwasababu Serikali imeshakuwezesha na tunatarajia kuona matokeo".

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Mhandisi Peter Ulanga alisema TTCL iko tayari kukamilisha miradi yote ya mawasiliano kwani Shirika hilo linatambua dhamira ya Serikali ya kuifanya Tanzania ya kidigitali ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ubora na zenye Uhakika.