info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TANZANIA YAPONGEZWA KWA MAFANIKIO YA KUPELEKA MAWASILIANO VIJIJINI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mohammed Khamis Abdulla, amesema kuwa Tanzania imepokea pongezi kutoka kwa mataifa mbalimbali ya Afrika kutokana na juhudi zake za kupeleka huduma za mawasiliano hadi maeneo ya vijijini, hatua iliyoiweka nchi kuwa mfano bora wa kuigwa barani Afrika.

Akizungumza wakati wa kufunga Mkutano wa 14 wa Jukwaa la Afrika la Utawala wa Mtandao (AfIGF 2025) uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam kuanzia Mei 29 hadi 31, 2025, Bw. Abdulla alisema kuwa mkutano huo ulihudhuriwa na washiriki kutoka karibu nchi 40 za Afrika na ulilenga kujadili maendeleo ya kidijitali katika bara la Afrika.

Amebainisha kuwa maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo yatawasilishwa katika Jukwaa la Dunia la Utawala wa Mtandao, ambapo Afrika itawakilishwa kwa msimamo mmoja kama bara.

Katika hotuba yake, Bw. Abdulla alizikaribisha nchi nyingine za Afrika kuja kujifunza kutoka Tanzania kuhusu namna ilivyofanikiwa kuwawezesha wananchi wake, hususan wale wa maeneo ya vijijini, kupitia huduma za mawasiliano.

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) lilishiriki kikamilifu katika maonesho ya teknolojia yaliyofanyika sambamba na mkutano huo, ambapo lilikuwa na banda maalum la kuonesha huduma zake mbalimbali. TTCL pia ilidhamini huduma ya intaneti kwa washiriki wa jukwaa hilo, hatua iliyochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha majadiliano na mawasiliano kwa urahisi katika kipindi chote cha mkutano.

.