TEMBELEA BANDA LA TTCL SABASABA KWA MAHITAJI YA HUDUMA ZA UHAKIKA SALAMA NA GHARAMA NAFUU -BI. MAEDA
Shirika la Mawasiliano Tanzania TTCL, ni miongoni mwa Taasisi, Kampuni Mashirika ya Umma na Binafsi pamoja na Wajasiriamali mbalimbali wanaoshiriki Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es Salaam huku shirika hilo likijipambanua kama muunganishaji thabiti likizingatia na usalama wa huduma za mawasiliano kwa wateja wake.
Akizungumza katika Maonesho hayo, Meneja wa Banda la TTCL, Bi. Janeth Maeda, ametoa wito kwa Watanzania na washiriki wa maonesho hayo kutembelea banda la TTCL ili kujionea huduma za kibunifu, zinazojibu mahitaji halisi ya sasa ya Taasisi, Mashirika na wananchi wa kawaida.
Bi. Maeda amesema Shirika hilo lipo katika maonesho hayo kuuhabarisha umma namna TTCL inavyotekeleza wajibu wake kwa Wananchi likiwa limeaminiwa na serikali na kupewa dhamana ya kusimamia na kuendesha miundombinu ya kimkakati ya serikali ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) na Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (NIDC).
"TTCL ni suluhisho la sasa na la baadaye katika huduma za TEHAMA. Hii ndiyo sababu Serikali imeendelea kutuamini kusimamia miundombinu ya kitaifa yenye umuhimu mkubwa kwa usalama wa Taifa na maendeleo endelevu ya kiuchumi," alisema Bi. Maeda.
Amesema kuwa TTCL inatoa huduma kwa Taasisi nyingi za Umma ambazo zimeonesha mafanikio makubwa katika utekelezaji wa majukumu na kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi.
Amezitaja taasisi hizo ni pamoja na taasisi za Kifedha, Wizara zote, Taasisi na Mashirika ya kiserikali, Sekta ya madini, sekta zisizo za kiserikali, sekta ya Afya na elimu, sekta ya usafirishaji pamoja na sekta ya utalii.
Bi. Maeda ameongeza kuwa kwa kutumia huduma za TTCL kupitia Mkongo wa Taifa, Mawasiliano, huduma za Kuhifadhi Data Kimtandao ndani ya nchi, na usambazaji wa mifumo ya TEHAMA, taasisi hizo zimepiga hatua kubwa katika kuongeza ufanisi, kupunguza gharama za mawasiliano na kuimarisha usalama wa taarifa zao.
"Kupitia teknolojia yetu ya fiber optic, tumeweza kuwahudumia mashirika haya kwa kasi ya kuaminika, jambo ambalo linaongeza tija na usalama katika utendaji wao wa kila siku," aliongeza Maeda.
Katika hatua nyingine Bi. Maeda anaawaalika Wananchi, Wadau wa biashara, Mashirika, Kampuni, na wageni kutoka Mataifa mbalimbali na Taasisi kufika kwenye banda la TTCL namba 26 ili Kujionea teknolojia ya mawasiliano ya kisasa inayowezeshwa na mtandao wa TTCL, kujifunza kuhusu namna bora ya kidigitali ya uhifadhi salama wa taarifa (Data Center), na kupata maarifa ya namna ya kupunguza gharama na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao.
Aidha amesema katika msimu huu wa sabasaba shirika hilo limeweka punguzo kubwa kwenye vifaa vya mobile ambavyo ni Router, USB modem, na MIFI kwa ajili ya kuwawezesha wateja kumiliki vifaa hivyo na kufurahia ulimwengu wa kidigitali katika kurahisisha mawasiliano.