TTCL YAENDELEA KUTOA ELIMU YA HUDUMA ZAKE KUPITIA REDIO UHURU
Na Adeline Berchimance
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) leo limefanya kipindi maalum kupitia Radio Uhuru FM, kwa lengo la kuwafikishia wananchi elimu kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na Shirika pamoja na fursa zinazopatikana kupitia teknolojia ya mawasiliano.
Akizungumza katika kipindi hicho, Meneja Mauzo na Usambazaji Bw. Leonard Laibu, ameeleza kwa kina kuhusu huduma na suluhisho mbalimbali zinazotolewa na TTCL, na namna wananchi wanavyoweza kutumia huduma za shirika hilo kupata fursa za ajira na kujiajiri.
Katika kipindi hicho, Laibu pia alitoa elimu kuhusu Mradi Faiba Mlangoni Kwako Awamu ya Pili, pamoja na huduma ya T-Burudani Plus namna wananchi wanaweza kunufaika huduma ya inataneti majumbani na manufaa ya ziada ambayo wateja wanaweza kupata kupitia huduma ya faiba.
“Tupo hapa kama shirika kupitia Redio Uhuru kutoa elimu inayolenga kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu thamani na fursa zinazopatikana kupitia huduma zinazotolewa na Shirika lao la mawasiliano” amesema Laibu.
Aidha amesema TTCL inao mchango na jukumu la kuunganisha watu, biashara na huduma za kidijitali ili kurahisisha utendaji wakazi na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa haraka na ubora unaotarajiwa.