TTCL YAENDELEA KUTOA FURSA YA MAFUNZO KWA VITENDO KWA WANAFUNZI KUTOKA VYUO MBALIMBALI NCHINI
Na Spencer Julius- Dar es salaam
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kutekeleza wajibu wake wa kijamii na kitaifa kwa kuwapokea wanafunzi kutoka vyuo na kada mbalimbali nchini kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo (Field Attachment) kwa mwaka wa masomo 2026/2027.
Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa TTCL wa kuchangia katika ukuaji wa taaluma na maarifa kwa vijana wanaosoma katika fani mbalimbali zinazohusiana na tasnia ya mawasiliano, teknolojia ya habari, uhandisi, biashara na fani nyingine za kitaaluma.
Lengo kuu la mpango huu ni kuwawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa vitendo utakaowasaidia kuunganisha nadharia waliyojifunza vyuoni na uhalisia wa mazingira ya kazi. Wanafunzi hao wamekuwa wakipitishwa katika idara na vitengo mbalimbali vya Shirika ili kujionea moja kwa moja jinsi TTCL inavyoendesha shughuli zake za kila siku, ikiwemo huduma za mtandao, miundombinu ya mawasiliano, huduma kwa wateja, na maeneo mengine ya kiutendaji.
TTCL inaendelea kutoa wito kwa vyuo na taasisi za elimu kuendelea kushirikiana na Shirika katika kuwajengea wanafunzi fursa za mafunzo kwa vitendo, huku ikisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuchangia katika maendeleo ya jamii kupitia elimu na maarifa.