
TTCL YAFANIKISHA KAMPENI YA FTTH KIMARA STOP OVER, YAHAMIA KIMARA TEMBONI
Meneja wa Kibiashara wa TTCL Mkoa wa Dar es Salaam Kaskazini, Bw. Diwani Mwamengo, amesema utekelezaji wa kampeni ya Faiba Mlangoni Kwako (FTTH) katika eneo la Kimara Stop Over umefanikiwa kwa kiwango cha kuridhisha, na sasa kazi inaelekezwa katika eneo la Kimara Temboni.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Bw. Mwamengo alieleza kuwa mwitikio wa wananchi wa Kimara Stop Over kujiunga na huduma ya FTTH umekuwa mkubwa, hali inayoonesha uelewa wa faida na ubora wa huduma hiyo.
“Tumepokea maombi mengi ya kuunganishiwa huduma na hadi sasa wateja zaidi ya 800 tayari wamefungiwa intaneti majumbani na kwenye biashara zao. Hii ni ishara kwamba wananchi wanatambua umuhimu wa huduma hii katika kuboresha maisha yao na shughuli zao za kila siku,” alisema Bw. Mwamengo.
Kuhusu hatua inayofuata, Bw. Mwamengo alisema tayari maandalizi ya kiufundi na uhamasishaji yameanza Kimara Temboni, ambapo wakazi wa eneo hilo wanatarajiwa kupata huduma yenye kasi kubwa, ubora wa kimataifa, na gharama nafuu.
Kwa mujibu wa Bw. Mwamengo, alisema upatikanaji wa huduma ya FTTH eneo la Kimara utaleta mapinduzi makubwa katika eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kuongeza ufanisi wa biashara ndogondogo na za kati (SMEs) kupitia miunganisho thabiti ya intaneti.
Aliongeza kuwa uwepo wa huduma hii utawawezesha wanafunzi na walimu kufaidika na elimu mtandaoni kwa urahisi Zaidi na kuboresha huduma za kijamii na mawasiliano ya kifamilia kupitia intaneti yenye kasi ya juu zaidi.
Aidha, alitoa wito kwa wananchi wote wa Kimara Temboni na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi kujiunga na huduma hii kwani ni fursa ya kipekee kwa kila familia, biashara na taasisi kujiunga na dunia ya kidigitali.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa kila kaya na biashara kujiunganisha na dunia ya kidijitali kupitia TTCL Business. Tusiruhusu uharibifu wa miundombinu kwani ni rasilimali ya wote na itahakikisha huduma inapatikana bila usumbufu,” alisisitiza.
Alisema kuwa Kampeni ya FTTH Kimara ni sehemu ya mkakati wa TTCL kupeleka huduma ya intaneti ya kasi kwa wananchi kote nchini, ikilenga kuchochea uchumi wa kidijitali na kuongeza ubora wa maisha ya Watanzania.