info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

TTCL YAFANIKISHA MKUTANO WA PAPU KIMTANDAO

Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL  ni miongoni mwa Taasisi na Mashirika ya Umma yaliyo chini ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari yaliyoshiriki maonesho yaliyoandaliwa na Wizara hiyo wakati wa Kikao cha 41 cha Baraza la Umoja wa Posta Afrika kilichofanyika jijini Arusha.

Meneja Biashara ambaye pia ni Meneja wa Banda katika maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa (AICC), Bw. Laibu Leonard  alisema moja kati ya faida ya kushiriki Maonesho hayo ni kuendelea kuifungua nchi katika sekta ya utalii kwani TTCL inaonesha matukio ya moja kwa moja yanayoendelea katika mlima Kilimanjaro.

Bw. Leonard alisema kupitia maonesho hayo nchi 30 kati ya nchi  wanachama 45 wa Umoja wa Posta Afrika (PAPU) zimenufaika na kasi ya mtandao iliyotolewa na TTCL na hivyo kuziwezesha kufanikisha matukio mbalimbali yanayohusu ajenda za Kikao hicho.

AlisemaTTCL imebeba dhamana ya kuhakikisha washiriki wote wanapata mtandao wa uhakika  na  kasi ili dhamira ya kikao hicho ya kufanya shughuli za Posta kufanyika kidigitali iweze kuonekana inatekelezeka.

"Shirika letu tunawaunganishia washiriki wote hapa Wireless ya bure yenye kasi ya 10G ni kasi ya uhakika na haikwamikwami na hapa pia tunaonesha Moja kwa moja matukio yanayoendelea katika mlima Kilimanjaro kwanzia mwanzo mpaka Uhuru Peak" alisema Laibu

Aliongeza kuwa kupitia maonesho ya Banda la TTCL ni wazi watavutiwa na upo uwezekano kwa baadhi ya wajumbe wakimaliza Mkutano wanaweza kwenda kutembelea mlima huo ili kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika Hifadhi ya mlima Kilimanjaro.

Aidha alibainisha kuwa kupitia Mkutano huo wa PAPU TTCL imepata fursa ya kuonesha huduma zake kwa wageni ambapo huduma hizo ni pamoja na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) huduma za Data Center (NIDC) hivyo washiriki wameweza kupata uelewa wa namna miradi hii ya kimkakati inavyosimamiwa na umuhimu wake kwa Wananchi.

Pia Leonard aliongeza kuwa Shirika hilo kama msimamizi na mwendeshaji wa miradi ya mawasiliano ya kimkakati linatekeleza majukumu yake ya kuhakikisha miundombinu ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano inajengwa nchini hadi nje ya mipaka ya Tanzania ili kuziwezesha shughuli za Posta ndani na nje ya Afrika kufanyika vizuri.

.