info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAIBUKA KINARA WA HUDUMA BORA ZA MAWASILIANO NCHINI

Na Spencer Kulwa

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetajwa kuwa kinara katika utoaji wa huduma bora za mawasiliano nchini, hatua inayothibitisha mafanikio ya uwekezaji wa muda mrefu katika miundombinu na mifumo ya huduma kwa wateja.

Hatua hii imekuja baada ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), kuwasilisha kwa waandishi wa habari ripoti ya robo mwaka inayoeleza hali ya Sekta ya Mawasiliano nchini, ambapo TTCL ilijitokeza kwa kiwango cha juu cha Ubora wa Huduma (Quality of Service - QoS) ikilinganishwa na watoa huduma wengine wa mawasiliano nchini.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Meneja Uhusiano wa Umma kutoka TTCL, Bi. Ester Mbanguka, amesema matokeo hayo ni tunda la uwekezaji uliofanywa katika miundombinu pamoja na mifumo ya ndani na nje inayorahisisha utoaji wa huduma kwa wateja kwa ufanisi na gharama nafuu.

"TTCL imekuwa kinara katika utoaji wa huduma bora za mawasiliano, haya ni matunda ya uwekezaji mkubwa uliofanywa katika Miundombinu ya Mawasiliano na huduma bora kwa Wateja," alisema Mbanguka.

Ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na jitihada za dhati za shirika za kuboresha mtandao wake wa mawasiliano, ikiwa ni pamoja na uwekezaji unaoendelea katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), ujenzi na uimarishaji wa minara ya mawasiliano, pamoja na uboreshaji wa mifumo ya kidijitali inayosaidia ufuatiliaji wa ubora wa huduma kwa wakati.