TTCL YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NA FINLAND KATIKA SEKTA YA TEHAMA
Na Godfrey Andafiche
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuimarisha ushirikiano wa kimkakati na Serikali ya Finland pamoja na kampuni ya teknolojia ya Nokia, kwa lengo la kuvutia uwekezaji, kuendeleza teknolojia bunifu na kufungua fursa mpya za biashara katika sekta ya TEHAMA.
Hayo yamebainishwa kupitia ziara ya ujumbe wa Serikali ya Finland, ukiongozwa na Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Anna Merrifield, uliopokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, pamoja na Menejimenti ya Shirika, jijini Dar es Salaam.
Majadiliano hayo yamelenga kupanua maeneo ya ushirikiano katika uwekezaji, teknolojia, maendeleo ya miundombinu ya mawasiliano na utekelezaji wa miradi ya pamoja itakayoongeza ufanisi na upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano.
Kupitia ushirikiano huu, TTCL inalenga kutumia utaalamu na teknolojia za kisasa kuimarisha miundombinu ya TEHAMA, kupunguza pengo la kidijitali na kuharakisha safari ya Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali hasa katika kuhakikisha huduma za faiba mlangoni kwako zinafikia wigo mpana wa watanzania.
#TTCL #DigitalTransformation #StrategicPartnership #DigitalEconomy #ConnectingTanzania