info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAIMARISHA USHIRIKIANO WA KIMKAKATI NCHINI UINGEREZA, YAFUNGUA FURSA ZA UWEKEZAJI NA MAENDELEO YA KIDIJITI

Na Emerco Mashelle

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa mikakati yake ya ukuaji na upanuzi wa huduma za mawasiliano, kupitia ziara ya kikazi nchini Uingereza iliyolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji na kutafuta fursa za kushirikiana katika miradi ya kimkakati ya Shirika.

Ziara hiyo, iliyofanyika jijini London kuanzia Oktoba 6 hadi 9, 2026, iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Bw. Moremi Marwa, akiambatana na ujumbe wa Shirika.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa TTCL ulifanya mikutano ya kimkakati na taasisi mbalimbali za kimataifa, zikiwemo UK Export Finance (UKEF), British International Investment (BII), Afreximbank, Invest Africa na Meta, kwa lengo la kujadili fursa za ushirikiano wa kibiashara, uwekezaji na ushirikiano katika miradi ya mawasiliano na teknolojia ya habari.

Majadiliano hayo yalijikita katika maeneo muhimu ya kimkakati, hususan upanuzi wa miundombinu ya Faiba Mlangoni Kwako (Fiber to the Home – FTTH), uendelezaji wa Kituo cha Taifa cha Data (National Data Centre), pamoja na fursa za ushirikiano katika uimarishaji wa miundombinu na huduma za kidijitali.

Hatua hiyo ni sehemu ya jitihada za TTCL za kutafuta fursa zinazoweza kusaidia kuongeza uwezo wa Shirika katika kutoa huduma za kisasa za mawasiliano, kupanua wigo wa biashara na kuimarisha ushindani wake katika soko la mawasiliano.

Aidha, ziara hiyo imetoa fursa ya kuimarisha mahusiano ya TTCL na taasisi za kimataifa zenye uwezo wa kushirikiana na Shirika katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuharakisha mageuzi ya kidijitali nchini.

Kufuatia ziara hiyo, TTCL inaendelea na hatua za ufuatiliaji wa majadiliano yaliyofanyika ili kutathmini na kuendeleza fursa za ushirikiano na uwekezaji zilizojitokeza, kwa lengo la kuhakikisha zinachangia ukuaji wa biashara, uimarishaji wa miundombinu na maendeleo endelevu ya Shirika.