TTCL YAJIPANGA KIKAMILIFU KUWAHUDUMIA WATEJA KATIKA MAONESHO YA 49 YA BIASHARA YA KIMATAIFA – SABASABA 2025
Watumishi wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) wameonesha maandalizi ya hali ya juu katika kuhudumia wateja na wageni mbalimbali watakaotembelea Banda la TTCL katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa yaliyoanza leo Juni 28, mwaka huu katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Sabasaba jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa Watumishi hao Bwana Emerco Mashelle alisema wamejiandaa kutoa huduma bora, majibu ya haraka kwa maswali ya wateja pamoja na kutoa elimu kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL.
Mashelle alisema maandalizi yao yamejikita katika kuhakikisha kila mteja atakayetembelea banda la TTCL ataondoka na uelewa sahihi kuhusu kazi, majukumu na mchango wa shirika hilo katika mapinduzi ya mawasiliano nchini.
Alisema katika msimu huu wa maonesho, TTCL imejipanga kutoa huduma mbalimbali kwa wateja ikiwa ni pamoja na huduma ya Faiba Mlangoni ambayo inampa fursa mteja kupata huduma ya Mtandao (intaneti) nyumbani kwake au ofisini kwa gharama nafuu huku ikimwezesha kuongeza ufanisi katika kazi zake.
Huduma nyingine ni mobile ambapo katika Msimu huu shirika hilo limeweka punguzo kubwa kwa ajili ya kuwawezesha wateja kumiliki vifaa hivyo vitakavyowawezesha kufanya majukumu yao kidigitali.
Aliongeza kuwa katika maonesho hayo wanatoa elimu na kuwajengea uelewa wateja Wakubwa kuhusu mifumo ya mawasiliano ya ndani ya ofisi (VPN), huduma za data center, pamoja na ufumbuzi wa kimawasiliano kwa Taasisi, Mashirika ya Umma na Binafsi.
Aliongeza kuwa Shirika limeunda timu maalum ya watumishi wenye taaluma mbalimbali waliopangwa kuhudumu ndani ya siku zote 16 za maonesho huku kila mmoja amepewa jukumu mahsusi kuhakikisha taarifa sahihi zinawafikia wateja wote kwa usahihi.