TTCL YAKABIDHI MAGARI 9 NA BAJAJI 28 KUIMARISHA UTOAJI WA HUDUMA
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Bw. Moremi Marwa, akabidhi rasmi magari tisa (9) na bajaji ishirini na nane (28) kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Shirika na kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika hafla iliyofanyika Makao Makuu ya Shirika hilo tarehe 29 Aprili 2026. Miongoni mwa waliokabidhiwa vyombo hivyo vya usafiri ni pamoja na Mkurugenzi wa Ufundi na Uendeshaji, Eng. Cecil Francis, Mkurugenzi wa Biashara, Bw. Vedastus Mwita, pamoja na Meneja wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, Bi. Esther Kamulali.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Bw. Marwa alisema kuwa Shirika limetumia jumla ya shilingi bilioni 1.6 kununua magari 9 aina ya Toyota Hilux, huku shilingi milioni 291.2 zikitumika kununua bajaji 28. Alieleza kuwa uwekezaji huo umetokana na faida iliyopatikana katika mwaka wa fedha 2024/25, ambapo TTCL ilirekodi faida ya shilingi bilioni 22.98.
“Uwekezaji huu unaakisi dhamira ya Shirika ya kurejesha faida kwa vitendo kupitia kuimarisha ufanisi wa kazi na utoaji wa huduma. Ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Kibiashara wa miaka 10 unaolenga kuongeza tija, kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma kwa wateja,” alisema Bw. Marwa.
Aidha, alibainisha kuwa vyombo hivyo vitasaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kiutendaji ikiwemo usimamizi na matengenezo ya Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB), utekelezaji wa mradi wa Faiba Mlangoni Kwako, pamoja na shughuli nyingine za kibiashara na kiufundi za Shirika.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ufundi na Uendeshaji, Eng. Cecil Francis, alimshukuru Mkurugenzi Mkuu kwa uwekezaji huo, akieleza kuwa utarahisisha utendaji kazi wa timu za kiufundi na kuongeza kasi ya utoaji huduma, hususan katika maeneo ya miundombinu.
Wakati huo huo, Shirika linatarajia kupokea magari mengine matano (5) mwishoni mwa mwezi Mei 2026, hatua itakayoongeza uwezo wa Shirika katika shughuli za masoko, mauzo na huduma kwa wateja.