info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAPANUA FURSA ZA BIASHARA ZA KIDIJITALI, YATUNUKIWA TUZO MKUTANO WA WAHANDISI

Na Debora Ngalima

 Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kujitanua katika fursa za biashara za kidijitali baada ya kutunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake katika kuwezesha na kufanikisha Mkutano wa 23 wa Wahandisi uliomalizika leo, Septemba 25, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo imekuja baada ya TTCL kuwezesha huduma za mawasiliano, ikiwemo intaneti ya kasi, katika mkutano huo uliowakutanisha zaidi ya wahandisi 4,000 kutoka taasisi za Serikali na sekta binafsi.

Kwa upande wa biashara, ushiriki wa TTCL katika mkutano huo umelipa Shirika hilo fursa ya kuonyesha uwezo wake wa kutoa huduma za mawasiliano kwa taasisi na sekta binafsi, katika kipindi ambacho shughuli nyingi za kitaalamu na kibiashara zinaendelea kuhamia kwenye mifumo ya kidijitali.

Kutambuliwa kwa mchango huo kupitia tuzo kunaweka msisitizo katika umuhimu wa huduma za mawasiliano zenye kasi, uhakika na uwezo wa kukidhi mahitaji ya taasisi zinazotegemea teknolojia katika uendeshaji wa shughuli zao.

Akizungumzia mafanikio hayo Meneja Mkoa wa TTCL Dar es Salaam Kaskazini, Aron Msonga, amesema kutambuliwa kwa TTCL ni sehemu ya kuimarisha ushirikiano na taasisi na sekta binafsi katika kutumia teknolojia kufungua fursa za kiuchumi.

“Tuzo hii ni utambuzi wa mchango wa TTCL katika kufanikisha mkutano huu, lakini pia inatupa nafasi ya kuonyesha uwezo wetu wa kutoa huduma za mawasiliano zinazokidhi mahitaji ya taasisi na sekta binafsi. Tunaona fursa kubwa katika ukuaji wa uchumi wa kidijitali na tutaendelea kuwa sehemu ya kuwawezesha wadau kutumia teknolojia kukuza shughuli zao,” amesema Msonga.

Amesema mahitaji ya huduma za mawasiliano kwa taasisi na biashara yanaendelea kuongezeka kutokana na matumizi ya mifumo ya kidijitali, hali ambayo inatoa fursa kwa TTCL kupanua huduma zake katika maeneo mbalimbali ya uchumi.

“Tunapoendelea kuona biashara na taasisi zikitumia zaidi mifumo ya kidijitali, hitaji la miundombinu ya mawasiliano yenye uhakika linaongezeka. Hii ni fursa kwetu kuendelea kutoa suluhisho zinazosaidia taasisi kufanya kazi kwa ufanisi na kuongeza tija,” amesema.

Kwa mujibu wa Msonga, TTCL itaendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu na huduma zake ili kukidhi mahitaji yanayobadilika ya wateja na kuongeza matumizi ya huduma za kidijitali nchini.

Mkutano huo wa siku tatu uliofanyika kuanzia tarehe 23 hadi 25 Septemba, ulifunguliwa na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb), na kufungwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya. Mkutano huo uliobeba kaulimbiu “Kukuza Ubunifu wa Uhandisi na Mageuzi ya Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu” uliipa TTCL fursa ya kuhusisha huduma zake na mahitaji ya wataalamu, taasisi na sekta binafsi katika matumizi na uendelezaji wa teknolojia.Kwa TTCL, tuzo hiyo inaongeza utambuzi wa Shirika katika eneo la huduma za mawasiliano kwa taasisi na matukio makubwa, huku ikiendelea kutafuta fursa za kibiashara zinazotokana na ongezeko la matumizi ya teknolojia na mabadiliko kuelekea uchumi wa kidijitali.