
TTCL YAPATA PONGEZI ZA VIONGOZI WA SERIKALI KWA HUDUMA BORA NA MAENDELEO YA MKONGO WA MAWASILIANO NANENANE 2025
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kupewa pongezi kutoka kwa Viongozi Waandamizi wa Serikali kufuatia mchango wake mkubwa katika kuimarisha huduma za mawasiliano na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.
Pongezi hizo zimetokea kupitia ziara za viongozi mbalimbali waliotembelea banda la TTCL kwenye Maonesho ya Kilimo ya Nanenane 2025 yaliyofanyika katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma.
Mmoja wa viongozi hao ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Suleiman Serera, ambaye alisema shirika hilo limekuwa likihakikisha linatoa huduma bora zenye ubunifu na gharama nafuu, na kwamba huduma ya Faiba Mlangoni Kwako imekuwa kiungo muhimu katika kuongeza ufanisi wa kazi kwa watumiaji wa huduma za kidijitali.
“Huduma ya Faiba Mlangoni imenisaidia sana katika kazi zangu za kila siku. TTCL mmefanya kazi nzuri sana kuboresha huduma zenu, na mimi kama mtumiaji ninashuhudia mabadiliko chanya,” alisema Dkt. Serera.
Dkt. Serera ambaye ni miongoni mwa watumiaji wa huduma hiyo, alielezea kuridhishwa kwake na maboresho makubwa ya huduma hiyo na akabainisha kuwa upatikanaji wa vifurushi vya gharama nafuu kutoka TTCL unatoa fursa kwa wananchi wa kipato cha kati na cha chini kunufaika na maendeleo ya kidijitali.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Bw. Ally Gugu, aliipongeza TTCL kwa mchango wake wa kimkakati katika maendeleo ya Kitaifa na Kikanda kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.
Bw. Gugu alipongeza TTCL kwa hatua madhubuti za kuunganisha Mkongo wa Taifa na mataifa jirani, hatua ambayo alisema inaimarisha si tu mawasiliano ya ndani bali pia ushirikiano wa kikanda katika nyanja ya teknolojia, usalama na uchumi wa kidijitali.
“TTCL inaonesha mfano bora wa namna taasisi za umma zinavyoweza kuchangia katika ajenda ya maendeleo ya Taifa. Kuunganisha Mkongo wa Taifa na mataifa jirani kunatoa fursa pana kwa uchumi wa kidijitali na kuimarisha usalama wa mawasiliano yetu,” alieleza Bw. Gugu.
TTCL hadi sasa imefanikiwa kuunganisha Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Kenya, Zambia, Malawi, Msumbiji, huku jitihada zikielekezwa katika kuunganisha mpaka wa Kalemie kwa ajili ya kuifikia Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Hatua hii inatarajiwa kuiweka Tanzania kama kitovu cha mawasiliano ya kikanda kwa Afrika Mashariki na Kati.
Kwa upande mwingine, TTCL imeendelea kutumia Maonesho ya Nanenane kama jukwaa la kuwaelimisha wananchi kuhusu faida za huduma za kisasa za mawasiliano, ikiwemo upatikanaji wa intaneti ya kasi, huduma za kifedha kwa njia ya simu, pamoja na kuunganishwa kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi na masoko ya bidhaa zao kupitia TEHAMA.