info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAPONGEZWA KWA KUUNGA MKONO AJENDA YA TANZANIA YA KIDIJITALI

Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Afya), Mhe. Dkt. Jafar Rajab Seif, amelipongeza Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa mchango wake katika kuimarisha miundombinu ya mawasiliano na kuunga mkono jitihada za Serikali za kujenga uchumi wa kidijitali kupitia utoaji wa huduma za kisasa za TEHAMA.

Mhe. Dkt. Seif ametoa pongezi hizo June 22.2026, alipotembelea banda la TTCL katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Park, jijini Dodoma.

Akiwa katika banda hilo, alipata maelezo kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na TTCL, ikiwemo usimamizi wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Kimtandao (National Internet Data Centre – NIDC), pamoja na huduma za Cloud Computing, ambazo zinaziwezesha taasisi za umma, sekta binafsi na wafanyabiashara kuhifadhi, kusimamia na kulinda mifumo na taarifa zao za kidijitali kwa usalama, ufanisi na uhakika.

Akizungumza baada ya kutembelea banda hilo, Mhe. Dkt. Seif amesema ameridhishwa na uwekezaji unaofanywa na TTCL katika miundombinu ya mawasiliano na teknolojia za kisasa, akieleza kuwa huduma zinazotolewa na Shirika zina mchango mkubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za umma na kuharakisha mabadiliko ya kidijitali nchini.

"TTCL inaendelea kutekeleza jukumu muhimu katika kujenga mazingira wezeshi ya matumizi ya teknolojia nchini. Uwekezaji huu unasaidia taasisi kuboresha utoaji wa huduma, kuongeza ufanisi na kuimarisha usalama wa taarifa za kidijitali," amesema Mhe. Dkt. Seif.

TTCL inaendelea kushiriki katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kuonesha huduma na suluhisho mbalimbali za mawasiliano na TEHAMA, zikiwemo Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), simu ya mkononi, T-PESA, NIDC, huduma za Cloud Computing, pamoja na huduma nyingine zinazochangia utekelezaji wa ajenda ya Serikali ya kujenga Tanzania ya Kidijitali.