info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAPONGEZWA USIMAMIZI BORA WA MIUNDOMBINU YA TEHAMA KUPITIA NIDC

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kupitia Kituo cha Taifa cha Utunzaji Data Kimtandao (NIDC) limepongezwa kwa namna linavyosimamia na kuendesha kituo hicho kwa ubora mkubwa na viwango vya kitaalamu. 

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA), Bw. Mohamed Makame, wakati wa ziara aliyofanya katika Kituo cha Taifa cha Utunzaji Data Kimtandao (NIDC), akiambatana na wajumbe kutoka vitengo mbalimbali vya ZCSRA.

Bw. Makame amesema kuwa ziara hiyo imelenga kujifunza namna kituo hicho kinavyoendeshwa, hatua za kiusalama zilizopo pamoja na fursa za kutumia huduma za uhifadhi na usimamizi wa data kwa taasisi za umma.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Utawala, Bw. Alex George, ameukaribisha ujumbe huo kutoka ZCSRA na kueleza umuhimu wa NIDC katika kulinda, kuhifadhi na kusimamia taarifa muhimu za taasisi za serikali na binafsi, sambamba na kueleza fursa mbalimbali zilizopo kwa taasisi zinazotumia kituo hicho.