info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YASHIRIKI KATIKA ZIARA YA KIKAZI NCHINI JAPANI KUJIFUNZA MBINU BORA ZA KUKUZA UBUNIFU NA TEKNOLOJIA

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeungana na ujumbe wa wataalam kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ziara ya kikazi nchini Japani, yenye lengo la kujifunza mbinu bora za kuendeleza ubunifu na kukuza kampuni changa (startups) kupitia teknolojia ya kisasa. 

Ziara hiyo imefanyika katika Kituo cha Ubunifu cha Tokyo kinachojulikana kama Tokyo Innovation Base (TIB ambacho kilianzishwa mwaka 2023 na Serikali ya Mji wa Tokyo, ni sehemu ya mkakati wa kuifanya Tokyo kuwa kitovu cha kimataifa cha ubunifu na teknolojia.

Kituo hicho kinatoa huduma mbalimbali zikiwemo ushauri kwa wajasiriamali, nafasi za ushirikiano kati ya sekta binafsi na umma, mafunzo ya kiufundi, pamoja na fursa za uwekezaji kwa kampuni changa zenye ubunifu wa kiteknolojia.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika tarehe 8 Oktoba 2025, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Mulembwa Munaku, alisema kuwa lengo la ziara hiyo ni kujifunza mifumo bora ya uendeshaji wa vituo vya ubunifu ili kuhakikisha uendelevu na matokeo chanya kwa jamii.

“Tunataka kujenga vituo vya ubunifu vyenye miundombinu imara, vinavyowezesha ushirikiano wa karibu kati ya Serikali, sekta binafsi na wabunifu,” alisema Bw. Munaku.

Serikali ya Tanzania kupitia Tume ya TEHAMA inaendelea na utekelezaji wa mpango wa kujenga vituo nane vya ubunifu (Innovation Zones) nchi nzima. Vituo hivyo vitatoa nafasi kwa wabunifu, wataalam wa teknolojia na wawekezaji kushirikiana katika kubuni suluhisho za kiteknolojia zitakazochochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

Ujumbe wa Tanzania katika ziara hiyo umejumuisha wataalam kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya TEHAMA, TTCL, Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA). 

TTCL katika ushiriki huu imejiimarisha kama shirika la kimkakati katika kukuza ubunifu, kuendeleza teknolojia ya mawasiliano, na kujenga msingi imara wa uchumi wa kidijitali  hapa nchini.