TTCL YASHIRIKI MAONESHO YA 50 YA BIASHARA YA KIMATAIFA SABASABA 2026
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linashiriki katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo, yaliyoanza tarehe 28 Juni 2026, yanaadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwake na yanaongozwa na kaulimbiu isemayo, "Maonesho ya Biashara ya Kimataifa 'SabaSaba' Fahari ya Tanzania," yakilenga kutoa jukwaa kwa taasisi za umma na binafsi kuonesha bidhaa, huduma, teknolojia na ubunifu unaochochea maendeleo ya biashara na uchumi wa nchi.
Katika Banda Na. 26, TTCL inaonesha huduma na suluhisho mbalimbali za mawasiliano na teknolojia ya kidijitali, ikiwemo Faiba Mlangoni Kwako (FTTH), Huduma za wateja wakubwa,simu za mkononi, T-PESA, Cloud Computing, FTTx Experience Centre, huduma za Call Centre, pamoja na suluhisho nyingine za TEHAMA zinazokidhi mahitaji ya wananchi, taasisi na wafanyabiashara.
Aidha, wageni wanaotembelea banda la TTCL wanapata fursa ya kutumia TTCL Public Wi-Fi, kupata elimu kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali za Shirika, pamoja na ushauri wa kitaalamu kutoka kwa wataalamu wa TTCL kuhusu suluhisho bora za mawasiliano na teknolojia.
Katika kipindi chote cha maonesho, TTCL imeandaa ofa maalum za Sabasaba, ambapo wateja wanapata punguzo la bei za modem na router, sambamba na fursa ya kujisajili na kupata huduma mbalimbali papo kwa papo.
Ushiriki wa TTCL katika maonesho hayo unaonesha dhamira ya Shirika ya kuendelea kusogeza huduma za kidijitali karibu na wananchi, kuongeza matumizi ya teknolojia za mawasiliano, na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga Tanzania ya Kidijitali.
TTCL inawakaribisha wafanyakazi, wateja na wananchi wote kutembelea Banda Na. 26 ili kujionea teknolojia za kisasa, kupata huduma, kujifunza kuhusu suluhisho za kidijitali na kunufaika na ofa mbalimbali zilizopo wakati wa maonesho.