info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YASUKUMA MAPINDUZI YA TEHAMA SEKTA YA KILIMO KUPITIA MAONESHO YA NANENANE

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) linaendelea kuonesha dhamira ya kuleta mageuzi ya kidijitali nchini kupitia ushiriki wake katika Maonesho ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni, Jijini Dodoma. 

Katika maonesho haya, TTCL limejikita kutoa elimu na huduma kwa wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi, likisisitiza matumizi ya teknolojia ya mawasiliano katika kuleta ufanisi na tija kwenye sekta hizo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Viongozi mbalimbali waliofika katika banda la TTCL walionesha kufurahishwa na juhudi mbalimbali zinazofanywea na shirika hilo za kuboresha teknolojia ya mawasiliano ili kuwawezesha wadau mbalimbali kutekelza majuku yao kidigitali.

Dkt. Vicent Mashinji Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, alitembelea banda la TTCL na kulipongeza shirika hilo kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano nchini kupitia Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa. 

Alisema kuwa TTCL imekuwa mhimili muhimu wa maendeleo ya sekta ya kilimo, kutokana na huduma zake ambazo zinasaidia wakulima kupata taarifa kwa haraka na kwa uhakika.

“TTCL mmepiga hatua kubwa katika kujenga miundombinu ya mawasiliano. Ninawasihi muharakishe pia mpango wa kupeleka mkongo hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwamba mpango huo utaimarisha ushirikiano wa kikanda na kuongeza mapato ya taifa kupitia huduma zenu,” alisisitiza Dkt. Mashinji.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Mawasiliano kutoka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Bw. Munaku Mulembwa, alipongeza TTCL kwa ubunifu na maendeleo makubwa iliyoyapata katika kutoa huduma bora kwa Watanzania. 

Bw. Mnaku alisema kuwa TTCL imeonesha mfano bora wa jinsi Taasisi ya Umma inaweza kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kupitia TEHAMA.

“Nimefurahishwa na mabadiliko ya kiteknolojia na huduma mpya mnazozitoa. TTCL imeonesha kuwa ni mtoaji muhimu wa huduma za mawasiliano nchini. Endeleeni kuongeza kasi ya kuwafikia wateja wa ndani na nje ya nchi,” alisema Bw. Mulembwa.

Akizungumza katika banda la TTCL, Meneja wa Banda Bi. Janet Maeda alisema kuwa shirika hilo limejipanga kutoa elimu ya kimkakati kuhusu matumizi ya huduma za mawasiliano ya kisasa kwa Wakulima, Wafugaji na Wavuvi, kwa lengo la kuwawezesha kufanya shughuli zao kwa ufanisi zaidi, kwa wakati, na kwa gharama nafuu.

“TTCL inawaletea wadau wetu elimu ya mawasiliano ya kisasa. Tunaonyesha kwa vitendo jinsi huduma za kidigitali zinavyoweza kuongeza tija katika kilimo, ufugaji na uvuvi. Tunaamini TEHAMA ni msingi wa mabadiliko ya kweli kwenye sekta hizi,” alisema Bi. Maeda.

Aidha, Bi. Maeda alieleza kuwa TTCL limeweka kipaumbele katika kuwawezesha wadau wa sekta ya kilimo kuunganishwa moja kwa moja na masoko, taasisi za kifedha, huduma za utabiri wa hali ya hewa, pamoja na wataalamu wa kilimo kwa kutumia huduma za intaneti ya kasi kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Alisema TTCL ni mshirika muhimu wa maendeleo, imeendelea kuunga mkono juhudi za serikali kwa vitendo kupitia utoaji wa huduma za intaneti ya kasi, elimu ya matumizi ya TEHAMA, pamoja na kuunganisha wadau na masoko ya kisasa kwa njia ya kidigitali.

Maonesho ya Nanenane 2025 yalifunguliwa rasmi tarehe 01 Agosti na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, yakiwa na kaulimbiu: “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.”