TTCL YATOA MAFUNZO YA HUDUMA BORA KWA MTEJA KWA TIMU YA MAFUNDI WA FAIBA MKOANI DODOMA
Na Spencer Julius
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kupitia Kitengo cha Uhusiano kwa Umma kutoka Makao Makuu, kwa kushirikiana na watumishi wa TTCL Mkoa wa Dodoma pamoja na kampuni ya Huawei, limefanikisha mafunzo maalum ya huduma bora kwa mteja yaliyolenga timu ya mafundi wanaotoa huduma ya uunganishaji wa intaneti ya Faiba Kwa wateja mbalimbali wa TTCL.
Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi za TTCL Mkoa wa Dodoma, yamekuja wakati ambapo Shirika linaendelea na utoaji wa Huduma ya "Faiba Mlangoni Kwako," inayolenga kuwafikia wateja moja kwa moja majumbani, maofisini na maeneo ya biashara kwa huduma za intaneti za kasi na uhakika.
Lengo kuu la mafunzo hayo ni kuendelea kuimarisha uhusiano bora baina ya TTCL na wateja wake, hususan wale wanaopokea huduma ya Faiba katika maeneo mbalimbali ikiwemo makazi ya watu, biashara na ofisini. Mafundi walioshiriki mafunzo haya ndio wanaobeba jukumu la moja kwa moja la kukutana na wateja wakati wa uunganishaji wa huduma, hivyo tabia na weledi wao una mchango mkubwa katika taswira ya Shirika mbele ya jamii.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Afisa kutoka Kitengo cha Uhusiano kwa Umma TTCL Makao Makuu, Bw. Emerco Mashelle alieleza kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa Shirika wa kuhakikisha kila mtumishi na mshirika anayewakilisha TTCL utendaji anazingatia weledi, heshima na ubora wa hali ya juu katika kuwahudumia wateja.
"Wateja wetu ndio msingi wa mafanikio ya Shirika hili. Ni muhimu kwa kila mmoja anayewakilisha TTCL mlangoni pa mteja - awe fundi, mtu wa mauzo au mfanyakazi yeyote - kuhakikisha anatoa huduma inayoendana na hadhi na jina la TTCL," alisema Mashelle.
Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Huawei alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kiufundi na kibiashara kati ya Huawei na TTCL katika kuhakikisha teknolojia inayotumika kutoa huduma ya Faiba inaendana na viwango vya kimataifa, huku ikizingatia pia namna bora ya kuwasiliana na wateja wakati wa usimikaji wa vifaa.
Huduma ya "Faiba Mlangoni Kwako" inaendelea mkoa wa Dodoma, ambapo wananchi wanahamasishwa kujiunga na huduma hiyo ya intaneti ya kasi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, biashara na ofisini.