info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

TTCL YATOA MSAADA WA VIFAA VYA USAFI SOKO LA MABIBO

SHIRIKA la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetoa vifaa vya kufányia usafi soko la Mabibo jijini Dar es Salaam kwa lengo likiwa ni kuunga mkono Wafanyabiashara Wanawake wanaofanya shughuli zao ndani ya soko hilo.

Msaada huo umetolewa na Wanawake wa Shirika hilo ni sehemu ya shamrashamra za Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo huadhimishwa kila Machi 8 kila mwaka. 

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa kwa Viongozi sokoni hapo Afisa Uhusiano wa Shirika la Mawasiliano Tanzania -TTCL Bi.Adeline Berchimance amesema Shirika limewaunga mkono Wanawake Wafanyakazi kutoa vifaa vya kufányia usafi kwa sababu eneo hilo hutumiwa zàidi na wanawake katika kununua mahitaji mbalimbali na Wanawake wengine ni miongoni mwa Wafanyabiashara na Wajasiriamali katika soko hilo.

"Tumekuja  mahali hapa ili kuwaunga mkono wanawake wenzetu wanaofanya shughuli za biashara sokoni hapa maana nimatamanio yetu kuwaona wakiwa katika mazingira safi na salama kwao hata kwetu sisi ambao ndiyo wateja wao wa kila siku"amesema Bi. Adeline.

Adeline amesema imekuwa ni utamaduni wa Menejimenti ya Shirika hilo kuwaunga mkono wanawake kila ifikapo Machi 8 kutoa msaada kwa wahitaji katika sekta  mbalimbali ikiwemo  Elimu na Afya. 

"Siku kama ya leo tuliwatembelea wagonjwa wa Saratani katika Taasisi ya Ocean Road Dar es Salaam na kutoa vitu mbalimbali" amesema .

Kwa upande wake Meneja wa soko la Mabibo Bw. Geoffrey Mbwama ameishukuru TTCL kwa msaada wao wa  vifaa vya kufányia usafi akisema utasaidia kuondoa changamoto iliyokuwepo ya ukosefu wa vitendea kazi sokoni hapo. 

"Hawa wanawake wa TTCL wametufanyia jambo kubwa sana na sasa mazingira haya yatakuwa masafi kama inavyotarajiwa." Amesema Bw. Mbwama

Ametoa wito kwa Watumiaji wa Soko hilo kuendelea kudumisha usafi kila wakati ili wananchi wanapofika kununua bidhaa wakute kuna mazingira safi na hata wale wanaouza bidhaa wauzie sehemu iliyo salama. 

Hata hivyo Meneja huyo ameziomba Taasisi na Masharika mengine kuiga mfano wa TTCL wa kukumbuka maeneo ya soko na kuyapa msaada.