TTCL YATUNUKIWA TUZO KWA MCHANGO WAKE KATIKA KONGAMANO LA KWANZA LA MWAKA LA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI NA FARAGHA
Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limetunukiwa tuzo ya kutambua mchango wake mkubwa katika kufanikisha Kongamano la Kwanza la Mwaka la Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Faragha, baada ya kudhamini huduma ya intaneti ya uhakika iliyowezesha shughuli zote za kongamano hilo kufanyika kwa ufanisi.
Tuzo hiyo ilitolewa na Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WMTH), Bi. Fatuma Zuberi Kalovya, wakati wa hafla ya kufunga kongamano hilo lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam Julai 1,2026, likiwakutanisha wadau kutoka sekta za umma na binafsi, wataalamu wa teknolojia, wasimamizi wa sheria pamoja na washirika wa maendeleo kujadili masuala ya ulinzi wa taarifa binafsi na faragha katika mazingira ya kidijitali.
Akizungumza wakati wa hafla ya kufunga kongamano hilo, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia amelishukuru Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa mchango wake mkubwa wa kudhamini huduma ya intaneti ya uhakika iliyowezesha shughuli zote za kongamano kufanyika kwa ufanisi.
Tuzo hiyo ni ishara ya kuthamini mchango wa TTCL katika kuendeleza matumizi ya teknolojia ya mawasiliano nchini na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga mazingira salama ya kidijitali yanayolinda taarifa binafsi za wananchi.
Mbali na kudhamini huduma ya intaneti, TTCL pia ilishiriki kikamilifu katika kongamano hilo kupitia wataalamu wake waliopata fursa ya kubadilishana uzoefu na wadau mbalimbali kuhusu masuala ya usalama wa mifumo ya TEHAMA, ulinzi wa taarifa binafsi na maendeleo ya teknolojia za mawasiliano endelevu za TTCL za kuimarisha uwezo wa kiutendaji wa Shirika na kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kutolewa kwa ufanisi, sambamba na utekelezaji wa mpango wake wa kimkakati wa kuimarisha huduma kwa wananchi.