info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAUNGANISHA DUNIA ARUSHA, YAWEZESHA MAWASILIANO IPU 2026

Na Debora Ngalima

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuonesha uwezo wake katika utoaji wa huduma za mawasiliano ya kisasa baada ya kuwezesha huduma za intaneti na mawasiliano katika Mkutano Mkuu wa 153 wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) unaofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC), jijini Arusha, kuanzia Oktoba 5 hadi Oktoba 9, 2026.

Mkutano huo mkubwa wa kimataifa umewaleta pamoja zaidi ya wajumbe 2,000, wakiwemo Maspika na Wabunge kutoka mataifa zaidi ya 180 duniani. Ajenda kuu ya mkutano huo ni pamoja na kuimarisha utawala bora, amani na ushirikishwaji wa jamii, pamoja na uchaguzi wa viongozi wapya wa Umoja huo.

Kupitia uwezeshaji wa huduma za mawasiliano katika mkutano huo, TTCL imeweka mazingira mazuri ya mawasiliano kwa wajumbe, waandaaji na wadau mbalimbali, hivyo kurahisisha upatikanaji na ubadilishanaji wa taarifa kwa haraka na kwa ufanisi katika kipindi chote cha mkutano.

Hatua hiyo inaonesha uwezo wa TTCL kuhudumia matukio makubwa yenye hadhira ya kimataifa na mahitaji makubwa ya mawasiliano ya kidijitali. Pia ni fursa muhimu kwa Shirika kuonesha uimara wa miundombinu yake na uwezo wa Tanzania katika utoaji wa huduma za kisasa za mawasiliano.

Akizungumzia ushiriki wa TTCL katika mkutano huo, Meneja wa TTCL Mkoa wa Arusha, Bw. Amani Kichere, amesema uwezeshaji wa mawasiliano katika Mkutano wa IPU 2026 unaendelea kuonesha nafasi ya Shirika katika kuunganisha Tanzania na dunia kupitia teknolojia.

“Ushiriki wetu katika Mkutano wa IPU 2026 unaonesha uwezo wa TTCL katika kuwezesha mawasiliano katika majukwaa makubwa ya kimataifa. Kadiri matumizi ya teknolojia yanavyoendelea kukua, tunatambua umuhimu wa kuwa na miundombinu imara na ya uhakika inayowawezesha watu, taasisi na biashara kuwasiliana kwa ufanisi,” amesema Kichere.

Kwa TTCL, mkutano wa IPU 2026 ni zaidi ya utoaji wa huduma za intaneti. Ni jukwaa la kuonesha namna teknolojia ya mawasiliano inavyoweza kuchochea diplomasia, biashara, ushirikiano wa kimataifa na maendeleo ya uchumi wa kidijitali.

Aidha, uwepo wa wajumbe kutoka mataifa zaidi ya 180 unaifanya Arusha kuwa kitovu muhimu cha mawasiliano ya kimataifa katika kipindi cha mkutano huo, huku TTCL ikiwa sehemu muhimu katika kuhakikisha shughuli mbalimbali za mkutano zinaendeshwa katika mazingira yenye mawasiliano ya uhakika.

Uwezeshaji wa mawasiliano katika Mkutano Mkuu wa 153 wa IPU unaongeza hatua nyingine katika safari ya TTCL ya kuimarisha nafasi yake katika majukwaa ya kitaifa na kimataifa, huku ikiendelea kutumia teknolojia kuunganisha watu, taasisi, biashara na kufungua fursa mpya katika uchumi wa kidijitali.

Kwa hatua hiyo, TTCL inaendelea kuunganisha Tanzania na dunia, huku Arusha ikiwa kitovu cha mawasiliano, diplomasia na ushirikiano wa kimataifa kupitia IPU 2026.