info@ttcl.co.tz
+255 22 210 0100

TTCL YAWAJENGEA UWEZO WANAFUNZI WA DIT KUHUSU UENDESHAJI WA MKONGO WA TAIFA WA MAWASILIANO

Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kukuza ujuzi wa teknolojia nchini kwa kutoa mafunzo ya kitaalamu kwa wanafunzi wa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) kuhusu uendeshaji na usimamizi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano.

Mafunzo hayo yalitolewa na wataalamu wa TTCL wakati wanafunzi hao walipotembelea Makao Makuu ya Shirika jijini Dar es Salaam kwa ziara ya mafunzo iliyolenga kuwajengea uelewa wa kina kuhusu huduma, teknolojia na miundombinu ya mawasiliano inayotumika nchini.

Katika ziara hiyo, wanafunzi walipatiwa historia fupi ya TTCL, kuanzia kuanzishwa kwake, hatua mbalimbali za maendeleo ilizopitia hadi kufikia nafasi iliyonayo sasa katika sekta ya mawasiliano. Pia walielezwa kuhusu mchango wa Shirika hilo katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kuchochea matumizi ya teknolojia za kidijitali na kusaidia maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Sehemu muhimu ya ziara hiyo ilikuwa ni kutembelea Kituo cha Uendeshaji wa Mtandao, maarufu kama Network Operations Center (NOC), ambacho ni kitovu cha ufuatiliaji na usimamizi wa miundombinu ya mawasiliano.

Wakiwa katika kituo hicho, wanafunzi walipata maelezo ya kitaalamu kuhusu namna Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unavyofuatiliwa na kusimamiwa saa 24 kwa siku, siku saba kwa wiki, ili kuhakikisha huduma za mawasiliano zinaendelea kupatikana kwa uhakika katika maeneo mbalimbali nchini.

Wataalamu wa TTCL pia waliwaeleza wanafunzi kuhusu mifumo inayotumika kugundua changamoto za kiufundi, kufuatilia mwenendo wa mtandao na kuchukua hatua za haraka pale hitilafu zinapojitokeza. Hatua hizo ni muhimu katika kuhakikisha wananchi, taasisi za Serikali, sekta binafsi na watoa huduma mbalimbali wanaendelea kupata mawasiliano yenye ubora na uhakika.

Ziara hiyo imewapa wanafunzi nafasi ya kuona kwa vitendo namna maarifa wanayopata darasani yanavyotumika katika mazingira halisi ya kazi. Aidha, imeongeza uelewa wao kuhusu teknolojia, mifumo na utaalamu unaohitajika katika uendeshaji wa miundombinu mikubwa ya mawasiliano.

Kupitia ziara hiyo, TTCL imeonesha dhamira yake ya kushirikiana na taasisi za elimu katika kuwaandaa vijana wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya sekta ya TEHAMA na uchumi wa kidijitali nchini.

Ushirikiano wa aina hii ni muhimu katika kupunguza pengo kati ya elimu ya darasani na mahitaji halisi ya soko la ajira, huku ukiwawezesha wanafunzi kupata mwanga kuhusu fursa mbalimbali za kitaaluma na ajira katika sekta ya mawasiliano.