info@ttcl.co.tz
+255 22 214 2000

TTCL YAWEZESHA INTANETI YA KASI KONGAMANO LA CONNECT 2 CONNECT (C2C) ZANZIBAR.

TTCL kama kitovu cha Mawasiliano imehakikisha huduma ya intaneti inapatikana katika kiwango cha juu katika Kongamano hilo la Kimataifa ili kuwawezesha Wadau wa Kongamano hilo kuperuzi kwa uharaka na urahisi zaidi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Mkurugenzi wa Biashara wa TTCL Bw.Vedastus Mwita amesema huduma hiyo ya intaneti imefanikiwa kutokana na uwepo wa Miundombinu imara inayotolewa na TTCL.

Alisema, "TTCL si tu kama mtoa huduma za mawasiliano ya simu bali kama mhusika Mkuu aliyepewa mamlaka ya kupanga, kujenga, kuendesha na kudumisha miundombinu ya kimkakati ya mawasiliano ya simu, ambayo inaweza kubadilika kulingana na mabadiliko ya kisasa ya kiteknolojia na miundombinu hiyo imeundwa ili kuendana na mwingiliano wa Waendeshaji ndani na nje ya Tanzania.

Aidha alisema kwa sasa TTCL imefanya mabadiliko makubwa katika Kuboresha utoaji wa huduma ambapo imehakikisha miundombinu ya Mawasiliano ya simu kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano (NICTBB) umeboreshwa ambapo kwa sasa unapakana na nchi 8.Mwita alisema TTCL inahakikisha Uhifadhi data kwa kutoa suluhisho na vifaa vya kutunza Data kwa kupitia kituo cha kutunza data Kimtandao (NIDC) kilichoidhinishwa na ISO.

Sambamba na hilo alisema TTCL inahakikisha inakuwa ndio Lango la huduma za E-serikali kwa kukaribisha miundombinu na huduma muhimu za ICT, Lango la usalama wa kitaifa wa kielektroniki kwa kuimarisha usalama na usalama wa sekta ya mawasiliano.

Kongamano hilo la siku mbili (06-07 Septemba 2023) linawakutanisha Wadau zaidi ya 250 wa Tehama ili kuelezana Ukuaji wa Teknolojia, fursa mbalimbali za Kibiashara pamoja na Ushirikano wa Kibiashara. Na lilifunguliwa tarehe 6 Septemba,2023 na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Khalid S. Mohamed na kufungwa tarehe 7 Septemba,2023 na Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape M. Nnauye (Mb)